Katika muendelezo wa kuwafikia wafanyabiashara wengi kuufahamu na kutumia Mfumo Mpya wa ukusanyaji wa Mapato Kwa njia ya dijitali ujulikanao kwa jina la TAUSI, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeongeza kasi ya utoaji wa elimu hiyo kupitia vituo mbalimbali vilivyopo kwenye Ofisi za Kata na Mitaa ya Halmashauri ya Jiji pamoja vituo vya Ofisi za TRA.
Akizungumza wakati wa ziara Maalum ya kutembelea Vituo hivyo, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Ofisi ya Rais - TAMISEMI Ndg. James Nicholas amesema kuwa lengo kubwa la ziara hiyo ni kutembelea na kujionea changamoto wanazopata katika zoezi la utoaji wa leseni kupitia Mfumo huo kisha Wizara ijue wapi kwa kuboresha "Naupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa jitihada hizi mlizochukua za kutenga Vituo Kumi (10) kwa ajili ya utoaji wa huduma za naombi ya leseni Kwa wafanyabiashara kwenye maeneo yao, tumeona changamoto kadhaa ikiwemo tatizo la Mfumo wenyewe hivyo tumeyachukua na tutayawasilisha kwa ajili ya utatuzi, lakini hakikisheni mnapowasajili muwaelekeze jinsi ya kutumia Ili baadaye waweze kutumia wenyewe kupata huduma kwakuwa ndiyo lengo kuu la Mfumo huu wa TAUSI" alisema Ndg. Nicholas.
Kwa Upande wake Afisa Biashara kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Ndg. Kefas Gembe, amewashukuru Maafisa hao kutoka TAMISEMI Kwa ujio wao kuona maendeleo ya zoezi la utoaji leseni Kwa Mfumo wa TAUSI na kusema kuwa Halmashauri ya Jiji imejipanga kutoa elimu Kwa njia zote kuhakikisha wafanyabiashara wanauelewa Mfumo huo mpya.
"Lengo letu ni kuwafikia wafanyabiashara wengi hivyo kupitia Vituo hivi zaidi ya Kumi (10) vya utoaji huduma za maombi ya leseni kwa Mfumo wa Tausi, naamini tutafikia Malengo tuliyojiwekea ya Ukusanyaji wa Mapato ya leseni za Biashara, Tunaomba Changamoto za kimfumo zifanyiwe kazi Ili tufikie Malengo Kwa Wakati" alisema Ndg. Kefas Gembe.
TAUSI ni mfumo mpya wa ukusanyaji wa Mapato kwa njia ya dijitali ambao unamrahisishia mfanyabiashara kufanya Malipo ya Halmashauri kwa njia ya mtandao kupitia simu yake ya kiganjani au kompyuta.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.