Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, imetoa elimu kwa wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Ilala, ambapo Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dkt. Elizabeth Nyema, amewashauri wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Ilala kupeleka Elimu ya Afya kwa wananchi wa Ilala.
Hayo ameyabainisha leo, wakati walipofanya kikao cha majadiliano baina ya wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya Jumuiya ya wazazi ya CCM Wilaya ya Ilala pamoja na Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
"Wakina Mama wengi huanza kliniki wakiwa na mimba ya wiki kumi na mbili na wengine wanakuja wakiwa wanakaribia kujifungua kwahiyo hata kama kuna tatizo nyuma hatuwezi kuligundua wakati mtoto ameshakua na kama hajapata dawa za awali kuweza kumkinga yeye na mtoto ikiwemo malaria inakuwa ni changamoto kwaiyo unakuta mama dakika za mwisho anapoteza mtoto lakini ni kwa sababu hakufika kliniki kwa wakati, tunaomba pia hii elimu iweze kufika ili iweze kuwasaidia akina mama na kupunguza vifo vya mama na mtoto" Alisema Dkt. Elizabeth Nyema.
Awali Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Ndugu Mtiti Mbassa Jirabi, alieleza kuwa eneo la Afya ni eneo ambalo limepewa kipaumbele katika kamati ya Wazazi ya Wilaya na kusisitiza Sekta ya Afya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuendelea kuwapatia elimu ili kuwawezesha nao kuisaidia Jamii
"Naomba nilisisitize hilo kama Sekta ya Afya itakuwa na utaratibu wa aina hiyo kutupatia elimu, sisi tunahitaji elimu kutoka kwenu ili tuweze kusaidia hizi jamii." alisema Jirabi
Aidha, Walter Kayombo, ambaye ni Mratibu wa Mfuko wa Afya ya Jamii (iCHF) Jiji la Dar es Salaam, alisema mwaka juzi walitenga milioni 6.4, kwaajili ya kuhudumia makundi maalumu yanayohusisha wazee, watu wenye ulemavu na wananchi wa kawaida wasio na uwezo wa kuhimili changamoto za matibabu, katika kiasi hicho cha milioni 6.4 kilichokuwa kimetengwa waliweza kutoa kadi 125 za utambuzi kwa wazee maeneo tofauti tofauti kwenye Halmashauri.
Naye Mratibu wa Malaria Jiji la Dar es Salaam, Ally Adinani, alisema kuwa lengo lao kubwa ni kupunguza Mbu waenezao malaria katika Jiji la Dar es Salaam "Tuna mbu ambao ni wengi na asilimia kubwa karibu 96% ni ‘curisense’ ambao ni mbu wasumbufu ambao wanaeneza mabusha na matende na 4% ni mbu wa malaria ambapo ukiangalia kimsingi wengi wako kwenye maeneo ya nje ya Jiji la Dar es Salaam" alisema AdnanI
Hata hivyo, Ndg. Adinani ametoa ufafanuzi kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepanga bajeti ya ununuzi wa viua mbu kwa mwaka huu kudhibiti maambukizi ya malaria katika Jiji la hilo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.