Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Eng. Amani Mafuru leo tar 28 Januari, 2023 amehitimisha mafunzo ya siku mbili ya Viongozi wa Wafanyabiashara wa Soko la Machinga yaliyoanza siku ya jana.
Akizungumza na Viongozi hao, Eng. Mafuru amesema amefarijika kuona wataalamu wakiwafundisha Wafanyabiashara hao uongozi na masuala mazima yanayohusiana na Fedha huku akiwataka wafanyabiashara hao kulipa kodi kwa wakati na kuwahaidi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itaongeza vituo vya kulipa kodi ili kupunguza kwenda umbali mrefu.
"Nafarijika sana nikiona sisi wote kwa pamoja tunafanya kazi kwa kushirikiana ili kuhakikisha kwamba Serikali inatimiza malengo yake ambayo imeyaweka na moja ni pamoja na semina hii" Amesema Eng. Mafuru.
Aidha, Eng. Mafuru amemshukuru Rais Samia kwa kuweza kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa Soko la Kariakoo na kusema tayari wameanza ujenzi wa Soko jingine jipya ili kuwe na uwiano wa idadi kubwa ya Wafanyabiashara waliopo na ukarabati wa soko la zamani la Kariakoo pamoja na Soko jipya unaridhisha kwani umefikia hatua nzuri.
"Mhe Rais amefanya jambo la kihistoria. Haikutarajiwa kama kutaweza kuwepo Soko lenye ghorofa nane, ghorofa sita kwenda juu na ghorofa mbili kwenda chini. Mkuu wa Mkoa alipewa wajibu wa kuhakikisha kwamba suala la Biashara na Wafanyabiashara katika Jiji la Dar es Salaam linafanyika bila kuleta athari ambapo moja ya maelekezo aliyotoa ni kuhakikisha Wafanyabiashara wanapewa elimu kama ambayo tumefanya leo.” Amesema Eng. Mafuru.
Aidha, Bi. Habiba Rajabu ambaye ni mfanyabiashara katika Soko la Machinga Complex amekiri Soko hilo kwa sasa linafikika kirahisi na watu wameweza kutambua uwepo wake na kupelekea Wafanyabiashara toka nchi jirani kulifahamu na kuja kufanya biashara kwenye Soko hilo.
Naye, Bw. Juma Malecha, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara Walemavu Mkoa wa Dar es Salaam aliishukuru Halmashauri ya Jiji la Dar esa Salaam chini ya Kaimu Mkurugenzi Eng. Amani Mafuru na uongozi mzima wa Machinga Complex kwa kuweka miundombinu rafiki kwa ajili ya walemavu.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.