Kamati ya Mifugo, Kilimo na Uvuvi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imefanya ziara ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo iliyotekelezwa na Halmashauri hiyo kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2023/2024 (Julai hadi Septemba 2023) ambapo leo tarehe 30 Oktoba, 2023 imetembelea miradi miwili ikiwemo eneo la kuuzia Maini na utumbo Vingunguti pamoja na ukaguzi wa eneo la muda la machinjio ya Kuku Kisutu.
Wakati wa ziara hiyo, Kamati iliweza kutembelea na kukagua eneo la soko la kuuzia maini na utumbo Vingunguti lenye jumla ya vizimba 66 na vizimba 25 ndivyo vinavyotumika kwaajili ya wafanyabiashara wa maini huku Soko la machinjio ya Kuku Kisutu likiwa na wafanyabiashara 133 ambao wachinjaji ni 64 na huchinja takribani kuku elfu moja kwa siku.
Akiongea wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Mifugo, Kilimo na Uvuvi Mhe. Abdulkharimu Masamaki ameishukuru Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kazi nzuri walioifanya kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya biashara zao katika maeneo rasmi na masafi hadi kuamua kuwatengenezea soko kwa ajili ya kuuza bidhaa zao huku akiwataka wataalamu kuhakikisha wanasimamia vizuri suala la miundombinu ya usafi kwa afya za wananchi.
Kwa upande wake Afisa Afya wa Soko la Maini na Utumbo Vingunguti Bw. Ally Kasembe ameeleza kuwa “Mradi huu umepunguza adha ya msongamano katika mabucha lakini eneo hili limekua dogo kwa wafanyabiashara hawa hadi kupelekea wafanyabiashara wa utumbo kuuza utumbo nje ya soko kwani miundombinu ya maji taka imekua ya shida katika soko letu hivyo tunaomba kuboreshewa miundombinu ya maji katika soko letu ili tuone namna bora ya kukuza biashara zetu na kupata mapato kwa wingi zaidi.”
Aidha, Kamati imependekeza kuwepo kwa mifumo ya maji taka katika soko la maini na utumbo Vingunguti au linunuliwe gari la kunyonya maji taka ambalo litasaidia kusafisha mazingira ya soko hilo kwa usalama wa afya za wananchi huku Kamati ikiagiza kuwepo kwa tozo ya uchinjaji katika machinjio ya kuku Kisutu kwani tozo hiyo itaongeza mapato ya Halmashauri ambayo yatapelekea kuboresha miundombinu yawafanyabiashara pamoja na kuendeleza miradi mingine ya maendeleo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.