Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Abbas Mtemvu leo Novemba 13, 2023 imepokea taarifa ya miradi na utekelezaji wa Ilani ya CCM iliyoambatana na ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Miradi iliyotembelewa na Kamati hiyo ni pamoja na ujenzi wa ghorofa Shule ya Sekondari Kimanga wenye gharama ya shilingi milioni 200 fedha kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ujenzi ukiwa hatua ya sakafu ya nne, Ujenzi wa ghorofa Shule ya Sekondari Liwiti uliogharimu shilingi bilioni 1.8 fedha kutoka mradi wa SEQIP pamoja na pochi la mama ujenzi ukiwa hatua ya ukamilishaji kwa jengo moja na hatua ya sakafu ya kwanza kwa jengo la pili, ujenzi wa madarasa 9 Shule ya Msingi Mnyamani unaotekelezwa kwa milioni 306 fedha kutoka mradi wa Boost ujenzi ukiwa unaendelea, ujenzi wa barabara ya Boom yenye urefu wa Km 0.44 iliyojengwa kwa kiwango cha lami yenye thamani ya shilingi milioni 654 Fedha kutoka TARURA ujenzi ukiwa umekamilika, pia Kamati iliweza kutembelea ujenzi wa ghorofa tatu Shule ya Msingi Diamond ambapo mradi huo unaotekelezwa kwa fedha kutoka mapato ya ndani shilingi milioni 200, fedha za mradi wa Boost shilingi milioni 142 pamoja na fedha za wahisani shilingi milioni 300 mradi huo ukiwa unaendelea na unatarajiwa kukamilika ndani ya Mwaka mmoja na nusu huku kamati ikimalizia ziara hiyo kukagua Mradi wa uwekaji wa vigae (Pavings) katika barabara ya Luthuli unaotekelezwa na fedha za mapato ya ndani kiasi cha shilingi milioni 517.9 ujenzi ukiwa unaendelea.
Akiongea wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Abbas Mtemvu amesema “Niwapongeze wataalamu wa Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa mradi kwani mmehakikisha fedha mlizozipokea zinatekeleza miradi kwa ufanisi na uweledi hivyo nimuagize Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi pamoja na wataalamu wa Halmashauri ya Jiji kuhakikisha mnawalipa wakandarasi kwa wakati na ikitokea Makandarasi anasua sua achukuliwe hatua ili miradi ikamilike kwa wakati uliopangwa."
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala Ndg. Said Sidde amesema “Naipongeza sana Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa utekelezaji wa miradi kwani thamani ya fedha inaonekana pia miradi inatekelezwa kwa kiwango cha juu zaidi hii inaonyesha ni jinsi gani Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inavyotekelezwa kwa kasi zaidi hivyo niwaombe mkamilishe miradi ya zamani kwa wakati na miradi mipya iendelee na ikamilike kwa wakati.”
Awali akiwasilisha taarifa ya miradi na utekelezaji wa Ilani kwa mwenyekiti wa CCM Mkoa pamoja na wajumbe wa kamati ya siasa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameeleza kuwa Wilaya ya Ilala ina Majimbo Matatu na Kata 36 zenye Jumla ya watu milioni 1.6 ambapo kutoka na wingi wa watu hao Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam imeendelea kuboresha sekta za Elimu, Afya pamoja na miundombinu ili kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Ilala wanapata huduma zote muhimu na kwa wakati.
Aidha Mhe. Mpogolo ameeleza kuwa “Zaidi ya shilingi bilioni 50 zimeletwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwaajili ya kuboresha Sekta ya elimu ikiwemo elimu ya awali, Msingi na Sekondari ambapo fedha hizo zimetumika katika ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa Mashuleni huku bilioni 8.7 zikiletwa kwaajili ya kuboresha miundombinu ya afya ambapo milioni 800 ni fedha kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri yenye lengo la kuendelea kuboresha sekta ya afya nchini huku shilingi bilioni 27 zikitolewa kuwezesha vikundi 1963 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu.”
Aidha Mhe. Mpogolo ameendelea kusema kuwa “Halmashauri yetu sasa katika jitihada za kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Jiji la Dar es Salaam tumeweza kuanzisha Kanda za huduma 7 ambazo zinasaidia wananchi kupata huduma kwa ukaribu zaidi ikiwemo vibali vya ujenzi pamoja na huduma nyingine muhimu ambapo baada ya kuanzishwa kwa Kanda hizo ongezeko la ukusanyaji wa mapato limeongezeka na hivyo kupelekea Halmashauri ya Jiji kutenga takribani Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa masoko makubwa ya Mchikichini, Ilala, Gongolamboto na Chanika pamoja na kuboresha mandhari ya Jiji letu.”
Kwa upande mwingine Mhe. Mpogolo amemshukuru Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salam kwa ziara aliyoifanya huku akimuhakikishia kutekeleza yote aliyoyaagiza.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.