Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo Aprili 30, 2024 imefanya ziara ya ukaguzi wa Miradi ya Afya lengo likiwa ni kufuatilia utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo zilizotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kipindi cha robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kilichoanza Januari hadi Machi 2024.
Ziara hiyo ililenga kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Afya inayoendelea kutekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kujionea maendeleo ya miradi hiyo jinsi itakavyorahisisha huduma mbalimabali za afya kwa Jamii pindi itakapokamilika.
Aidha, Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Chanika uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 107 ujenzi ukiwa katika hatua ya umaliziaji, ujenzi wa jengo la mionzi (X-Ray) Kituo cha Afya Pugu uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 107 utekelezaji wa mradi ukiwa hatua ya ukamilishaji pamoja na uwekaji mashine ya mionzi huku ujenzi wa ghorofa 5 Kituo cha Afya Mchikichini ukiwa umekamilika kwa asilimia 40 ambapo sakafu mbili zimekamilika na sakafu ya tatu imeanza kujengwa.
Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Saady Khimji amesema kuwa “Leo tumetembelea baadhi ya Miradi ya Afya inayosimamiwa na kutekelezwa na Halmashauri ya Jiji la DSM ambapo tumeweza kuridhishwa na utekelezaji huo hivyo nitoe wito kwa Watendaji wa Halmashauri kusimamia miradi hii kwa ukaribu zaidi na Sisi kama wasimamizi tutaendelea kushirikiana nao kuhakikisha miradi hii inatekelezwa kwa wakati na thamani ya Fedha inayotumika inalingana na ubora wa miradi kwani Kamati hufanya ziara hizi kwa lengo la kukagua na kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali Kuu pamoja na Halmashauri zinawafikia walengwa na kufanya kazi kama ambavyo fedha hizo zimeelekeza. Hivyo naomba mapungufu yaliyoonekana kwenye miradi hii yashughulikiwe kwa wakati ili wananchi wote wafikiwe na huduma muhimu na bora kwa wakati kama Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anavyoonesha juhudi zake katika kuwahudumia Wananchi.”
Sambamba na hilo Mhe. Khimji ameendelea kusema ni wajibu wa kila Mtendaji kuhakikisha anasimamia vyema shughuli za maendeleo ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo ya pamoja kwa Jamii
“Sera ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati kwani sisi kama wasimamizi hatutavumilia watu wanaokwamisha kwa makusudi miradi ya maendeleo hivyo nipende kutoa wito kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam kuhakikisha anashirikiana na watendaji wake kwa ukaribu kusimamia miradi hii ya afya ikamilike kwa wakati uliopangwa lengo ni kuwasaidia wananchi wetu kupata huduma bora kwa wakati. Pia tusisahau kuwashirikisha wananchi katika kufanikisha miradi kwani miradi hii inawalenga wao moja kwa moja." Amesisitiza Mhe. Khimji.
Aidha, Wajumbe wa Kamati wameridhia kuwa endapo kutakua na changamoto wakati wa utekelezaji wa miradi ni vyema changamoto hizo zikawasilishwa sehemu husika mapema na kufanyiwa kazi ili maendeleo ya wananchi yasikwamishwe huku wakiagiza wahandisi kutoka Halmashauri kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu zaidi ujenzi wa Miradi ya Maendeleo ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na iwe yenye ubora.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.