SERIKALI ya Mkoa wa Dar es Salaam imejipanga kuwaandaa wananchi na wafanyabiashara wake katika kuanza kufanya biashara za masaa 24 katika soko la Kimataifa la Kariakoo.
Katibu Tawala Mkoa wa Dar es salaam, Dkt. Toba Nguvila ameeleza hayo leo Februari 25, 2025 wakati wa usafi ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea uzinduzi wa biashara hizo, akisisitiza biashara hizo zinakwenda sambamba na usafi ili mazingira yake yaakisi hadhi ya kuwa soko la kimataifa.
Dkt. Nguvila amesema kuwa katika maandalizi hayo wamejipanga kufanya semina mbalimbali kwa ajili ya wafanyabiashara zikiwemo na watu wa Bima na Taasisi za kifedha zikiwemo benki ili kuwasaidia kuweza kujikinga na majanga kama moto pia waweze kukuza biashara na mitaji yao kupitia elimu ya kifedha.
Ameongeza kuwa kutakuwa na semina kutoka kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kuwapa elimu ya ulipaji kodi na hizo zitaanza kutolewa kesho saa 3:00 asubuhi hadi jioni na kuongeza kuwa itaendelea hadi hapo keshokutwa kwa wamachinga na wafanyabiashara wengine ambao hawatoweza kuhudhuria siku ya leo.
“Kesho kutakuwa na semina mbalimbali kwa wafanyabiashara wa soko la kariakoo ambao zitatolewa na wataalamu mbalimbali wakiwemo wa TRA kwa ajili ya masuala ya kikodi, wa bima kama mnavyoonda kariakoo kumetokea majanga ya moto na majengo kubomoka sasa ni wakati wa wafanya biashara kukata bima ili majanga yakitokea mitaji isiweze kukatika,” amesema Dkt. Nguvila.
Akizungumza kuhusu suala la usalama, Dkt. Nguvila amesema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga na kujiimarisha ulinzi ipasavyo na wanaendelea kuimarisha ulinzi mwingine wa mazingira kwa kufunga taa na kamera katika maeneo hayo kuhakikisha wafanyabiashara wa ndani na nje wanafanyakazi katika hali ya usalama.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.