Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Rehema Madenge leo Oktoba 30, 2023 ameshiriki katika Kikao cha Manejimenti kuongea na Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam pamoja na kufanya ziara ya ukaguzi wa Miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake katika kufanya ukaguzi wa kawaida wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kupima utendaji kazi.
Aidha, Bi. Rehema aliweza kukagua ukarabati wa ukumbi wa Karimjee, eneo la uwekaji wa vigae (pavings) kwenye njia ya watembea kwa mguu Kata ya Kivukoni ambapo takribani shilingi milioni 600 Fedha kutoka Mapato ya Ndani ya Halmashauri zimetumika kuteleza mradi huo unaoendelea katika Mitaa ya Luthuli, Sokoine na Ardhi pamoja na kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Mchikichini.
Akiongea wakati wa ziara hiyo Bi. Rehema amemshukuru Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na wataalamu wake kwa kuboresha na kupendezesha mandhari ya Jiji kwani kupitia mradi huo wa kuweka vigae Jiji la Dar es Salaam litazidi kuwa safi na mandahari ya Jiji itapendeza jambo ambalo litazidi kuwavutia watalii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Ndg. Jomaary Satura ameeleza kuwa “Katika kutekeleza Kampeni ya 'Safisha Pendezesha Dar es Salaam' tumeona ni vyema maeneo yote ya 'Smart Area' kuyawekea vigae ili kupendezesha Jiji letu pamoja na kuliweka katika hali ya usafi hivyo kwa kutumia fedha za mapato ya ndani maeneo yote ya Smart Area kuanzia Lumumba, Karimjee hadi Kivukoni tunaendelea kuyaboresha huku kwa upande wa Botanic Garden tukiwa tumeandaa ramani ya namna tutakavyopaboresha na watu kuweza kupumzika na ni matarajio yetu hadi kufikia Disemba 2023 miradi hii itakua imekamilika.”
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.