Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Suleiman Jafo (Mb) ameelekeza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha Kituo Kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani katika eneo la Mbezi Luis kinaanza kutumika muda wowote kuanzia sasa baada ya kujiridhisha kukamilika kwa miundombinu yote muhimu kasoro barabara ya kuingia kituoni hapo ambayo ipo hatua ya mwisho.
Waziri Jafo amesema hayo leo tarehe 25 Januari, 2021 wakati alipofanya ziara katika Kituo hicho ambapo amesema muda wowote ambao Wakala wa Barabara Tanzania “TANROAD” watathibitisha kuwa barabara ya kuingia kituoni hapo imekamilika ni vyema kituo kikaanza kutoa huduma.
Aidha Waziri Jafo amesema kutokana na Kituo kuwa na hadhi ya Kimataifa anapendekeza kipewe jina la Rais Dkt. John Magufuli kama sehemu ya shukrani na kuthamini jitihada anazofanya ambapo amesema atamuomba Mheshimiwa Rais aridhie ombi hilo.
Hata hivyo Waziri Jafo amemuelekeza Mkandarasi anayejenga eneo la maegesho ya magari madogo kuhakikisha anakamilisha kazi ndani ya majuma mawili kuanzia leo huku akitaka taa zifungwe ndani ya juma moja kuanzia leo.
Pamoja na hayo Waziri Jafo ametoa pongezi kwa uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa usimamizi madhubuti uliosaidia Kituo hicho kukamilika kikiwa na ubora uliokusudiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Sipora Liana amesema kazi zinazoendelea kwa sasa ni ufungaji wa viyoyozi, lifti, ufungaji wa taa na vifaa vya matangazo, uunganishwaji wa maji kwenye vyoo na miundombinu mingine ambayo nayo ipo hatua ya mwisho kukamilika na kusisitiza kuwa kwa sasa Kituo kinaweza kuanza kutumika
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.