Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo tarehe 19 Juni, 2019 wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji wameadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kufanya usafi katika Kituo cha Mabasi Ubungo pamoja na kuwajulisha wananchi na wadau kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mabasi katika eneo la Mbezi Luis ambako huduma za usafiri wa ndani na nje ya nchi zitahamishiwa kutoka Kituo cha sasa Ubungo.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Herman L. Msuha alieleza kwamba ujenzi na usimamizi wa Kituo cha Kimataifa cha Mbezi Luis umezingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ili kuweza kutoa huduma bora za usafiri ndani na nje ya nchi na kuwatoa hofu wadau wa Kituo cha Mabasi Ubungo.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji alihitimisha maelezo yake ya ufafanuzi kwa kuwakaribisha wananchi na wadau mbalimbali kutembelea eneo la Mbezi Luis kujionea maendeleo ya ujenzi wa Kituo kipya cha Kimataifa cha Mabasi pamoja na maonesho ya wajasiriamali katika Viwanda Vidogo Vidogo vya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam vilivyopo eneo la Mwananyama katika Manispaa ya Kinondoni, jirani na Hospitali ya Mwananyamala kuona kazi zinazofanywa na wajasiriamali hao ambao ni wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Wananchi na wadau mbalimbali wa Kituo cha Mabasi cha Ubungo wamepata fursa ya kuwasilisha hoja mbalimbali kuhusu huduma ya usafiri ndani ya Kituo pamoja na maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mbezi Luis na kupatiwa ufafanuzi wa hoja hizo.
Maadhimisho haya ni kwa mujibu wa kalenda ya Umoja wa Afrika (AU) ambapo nchi wanachama huadhimisha kwa kushiriki shughuli mbalimbali zinazohusu Utumishi wa Umma yanaratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora yakiwa na Kauli mbiu: "Uhusiano kati ya uwezeshaji wa vijana na usimamizi wa masuala ya uhamiaji: Kujenga utamaduni wa Utawala Bora, matumizi ya TEHAMA na ubunifu katika utoaji wa Huduma Jumuishi."
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.