Jiji la Dar es Salaam, leo tarehe 10 Juni, 2022, limepokea ujumbe wa Madiwani na Watendaji wapatao 26 kutoka katika Halmashauri ya Mjini Magharibi B, Zanzibar waliofanya ziara ya kujifunza namna ya uendeshaji wa Serikali za Mitaa.
Ujumbe huo ulioongozwa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Mjini Magharibi B Khamisi Haji, ulifika kujifunza mfumo wa ukusanyaji mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato vya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, utunzaji wa mazingira, jinsi Dar es Salaam ilivyofanikiwa kuwapanga wafanyabiashara ndogo ndogo katika masoko na sheria mbalimbali zinazotumika katika utendaji kazi.
Katika ziara hiyo ya siku tatu, ujumbe huo ulitembelea Soko Kuu la Kisutu, Soko la Buguruni na Soko la Machinga Complex. Eneo jingine walilotembelea ni kituo cha uchakataji taka taka kilichopo Kata ya Bonyokwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mjini Magharibi B, Khadija Simai, amesema kuwa wamejifunza mambo mengi mazuri ambayo hapo awali walikuwa hawayafahamu hivyo kwa namna moja au nyingine yatabadilisha utendaji wao wa kazi na kuleta matokeo chanya katika Halmashauri yao.
“Tumejifunza mambo mengi ambayo tulikuwa hatuyafahamu hapo awali. Tumejifunza namna bora ya ukusanyaji wa mapato, usimamiaji wa masoko, usimamiaji wa sheria ndogo ndogo za ukusanyaji wa mapato, namna bora ya kuwapanga wafanyabiashara ndogo ndogo katika masoko ili iwe rahisi kukusanya ushuru na namna bora ya utunzaji wa mazingira. Nina imani haya yote tuliyojifunza tukiyaweka kwenye utekelezaji tutakuwa tumepiga hatua kubwa.” Amesema Mkurugenzi huyo.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekuwa ikipokea wageni mara kwa mara kutoka ndani na nje ya nchi wanaokuja kujifunza namna inavyotekeleza majukumu yake na kupata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali kama ukusanyaji mapato.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.