Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), amewataka watanzania kuwajibika kulipa kodi kwa kutoa na kudai risiti ya Mashine za Kieletroniki (EFD), ili kuhakikisha mapato ya nchi yanaongezeka na kusaidia kutekeleza miradi na huduma mbalimbali za kijamii.
Mhe. Chande, ametoa rai hiyo leo Septemba 30, 2023 wakati wa hafla kufunga wiki ya EFD iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato TRA wakishirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala yenye kauli mbiu isemayo ‘EFD, Risiti yako, Ulinzi wako, iliyokuwa ikifanyika viwanja vya Jakaya Youth Park Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo pamoja na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Machinga Mhe. Chande amesema “Nitoe wito kwa wafanyabiashara kushirikiana kikamilifu na mamlaka husika kutumia mashine hizi kwa usahihi ili kufanikisha adhma ya ulipaji kodi kwa maendeleo ya nchi yetu kwani kila mtanzania anapaswa kuwajibika katika kulipa kodi na kudai risiti halali ya kieletroniki kila anapofanya manunuzi lengo likiwa ni kuhakikisha tunazuia upotevu wa mapato hivyo niwaombe TRA kukusanya mapato halali bila usumbufu kwa wafanyabiashara”.
Aidha Mhe. Chande ameendelea kusema “Tuendelee kushirikiana kwa pamoja, na yule ambaye halipi kodi basi awe na utamaduni wa kulipa kodi kwa maslahi mapana ya Taifa letu na Serikali itawajibika kuleta maendeleo kwa wananchi wake, nanyi muwajibike kulinda na kuhifadhi miradi ya maendeleo inayoletwa na Serikali yenu”.
Naye Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Ndg. Alphayo Kidata ameeleza kuwa “Tumeandaa wiki hii ya EFD lengo likiwa ni kutoa elimu kwa Wafanyabiashara na Wananchi wote kwa ujumla juu ya matumizi sahihi ya EFD na kuhakikisha wanalipa kodi kwa wakati huku Wananchi wakihakikisha wanadai risiti kila wanaponunua bidhaa na Wafanyabiashara kutoa risiti kila wanapofanya malipo hivyo niwahimize muwe na utamaduni wa kutunza kumbukumbu zetu za EFD wakati mnapotoa risiti pia mfanye maisha yenu yawe ya kulipa kodi kwani kodi ni msingi wa maaendeleo ya nchi yetu”.
Hafla hii ya ufungaji wa Wiki ya EFD iliambatana na Sport Bonanza ambapo timu za wafanyabiashara, machinga pamoja na TRA Ilala na Kariakoo waliweza kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo Mpira wa Miguu, kukimbia na vijiko, kuvuta Kamba, kukimbia na magunia pamoja na mchezo wa kuweka tenesi ndani ya bomba ambapo washindi wa michezo hiyo waliweza kupewa zawadi mbalimbali ikiwemo medali pamoja na Vikombe.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.