Na: Hashim Jumbe
"Sisi tumekwisha uwasha Mwenge, tumekwisha uwasha Mwenge. Na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro. Kuwasha Mwenge na kuuweka Kilimanjaro"
Naam, huo ni mpangilio wa sauti za kizalendo zilizobeba maudhui ya wimbo wa kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru, sauti kutoka kwa Vijana wa Halaiki wa Wilaya ya Ilala, ziliposikika asubuhi ya leo ya Tarehe 18 Agosti, 2021 kwenye viwanja vya ndege vya Dar es Salaam (terminal one) zikiashiria kuwa Mwenge wa Uhuru umewasili ndani ya viunga vya Wilaya ya Ilala
Aidha, wakati wa makabidhiano ya Mwenge huo wa Uhuru, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Luteni Mwambashi alisisitiza kuwepo kwa nyaraka na vielelezo vyote muhimu kwenye miradi ya Mwenge watakayoitembelea, huku Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija akieleza kwa ufupi miradi watakayotembelea na kuifanyia ukaguzi pamoja na kuweka mawe ya msingi "katika Wilaya ya Ilala, Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 zitapitia jumla ya miradi ya maendeleo 9 yenye jumla ya thamani ya Shilingi Bilioni 46.8"
Miradi iliyotembelewa kwa Wilaya ya Ilala ni pamoja na miradi Miwili (2) ya Vikundi vya uzalishaji mali vya vijana ambapo miradi hii imewezeshwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia mkopo wa asilimia 10% ya mapato ya ndani pamoja na kituo cha Mifumo ya TEHAMA 'Buguruni'
Mradi mwingine ni uboreshaji wa miundombinu ya ujenzi wa barabara ya lami, Stendi ya Kinyerezi na daraja la Ulongoni B ambao umewekwa jiwe la msingi, Mradi wa ujenzi wa madarasa ya ghorofa Shule ya Sekondari Ilala-Kasulu, mradi wa ujenzi wa kituo cha Polisi Mzinga ambao umetekelezwa kwa nguvu ya Wananchi na wenyewe umewekewa jiwe la msingi.
Vilevile mradi wa afya wa wadau ambao ni ujenzi wa Hospitali binafsi ya AL-AMAL uliopo chini ya Asasi ya Direct Aid Society (DAS) inayojulikana kwa jina la Africa Muslims Agency na wenyewe umewekewa jiwe la msingi na mradi wa utengenezaji wa samani za chuma wa kikundi cha DAGE cha Watu wenye Ulemavu kutoka kata ya Vingunguti ambao umewezeshwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia mkopo wa asilimia 10% ya mapato ya ndani, mradi huu umetembelewa na kukaguliwa na pia mbio za Mwenge zilikagua mradi wa mwaka 2019 kuona maendeleo yake, mradi huo ni ujenzi wa Tanki la kuhifadhia maji lita Milioni 2 lililopo Pugu
Aidha, wakati akitoa Salamu na Ujumbe wa Mwenge wa Uhuru 2021 kwa Wananchi wa Wilaya ya Ilala, Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Luteni Josephine Paul Mwambashi, Mwambashi alielezea mambo muhimu likiwemo la matumizi ya malipo ya kietroniki katika ukusanyaji wa mapato kwa ngazi ya Halmashauri, huku akiwaasa Wananchi kutokufanya malipo bila ya kupewa risiti ya EFD kwani kutokuchukua risiti kunaipunguzia Serikali mapato, lakini pia alisisitiza juu ya madhara ya madawa ya kulevya, huku akihimiza matumizi ya lishe bora ili kujenga jamii imara na kuendelea kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI ili kuikinga jamii yetu.
Mbio za Mwenge wa Uhuru 2021 zimebeba ujumbe unaosisitiza matumizi ya TEHAMA katika kuchochea maendeleo "TEHAMA ni Msingi wa Taifa Endelevu, Itumike kwa Usahihi na Uwajibikaji".
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.