Na: Hashim Jumbe
TAREHE 10 Oktoba, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alizindua kampeni ya Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19, ambapo katika uzinduzi huo uliofanyika Mkoani Dodoma Mhe. Rais alizitaka Taasisi zitakazonufaika na fedha za mkopo wa Shilingi Trilioni 1.3 kutoka IMF kuhakikisha zinatumika katika malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, fedha hizo zilizogawiwa kwa Halmashauri zote nchini zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii kwenye sekta za afya, elimu, maji na utalii, hivyo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imenufaika kwa kupata fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 5.1 zitakazotumika kujenga vyumba vya madarasa 255 ya sekondari.
Katika kuhakikisha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatekeleza mpango huo kwa wakati na kwa viwango vilivyowekwa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Jumanne Shauri, leo tarehe 27 Oktoba, 2021 alikutana na Wakuu wa Shule za Sekondari pamoja na Waratibu wa Elimu Kata ili kuweza kutengeneza mpango wa pamoja kufanikisha ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa unakamilika kabla ya tarehe 15 Disemba, 2021.
Akiongea katika kikao kazi hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Karimjee, Ndugu Jumanne Shauri aliwaasa Wakuu hao wa Shule za Sekondari kusimamia kwa uadilifu ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa ya sekondari vinavyojengwa kwenye shule 40 za Jiji la Dar es Salaam.
"Kuna vitu vya kuwekana sawa, naomba kwanza Afisa Elimu Sekondari atengeneze mpango kazi wa pamoja kuanzia leo tarehe 27 Oktoba, 2021, lakini pia Wakuu wa Shule niwaombe mtafute mafundi waliowazuri na 'Suppliers' wasio wababaishaji"
Ndugu Shauri aliendelea kusema "Hakikisheni kwenye eneo la plasta, tafuteni watu ambao ni wazuri, watapiga plasta na rangi vizuri, maana mnaweza kujenga jengo zuri sana alafu kwenye umaliziaji pasionekane vizuri, tafuteni mafundi ambao ni wazuri, tunataka madarasa ya Jiji la DSM yawe mfano kwa wengine waje kujifunza"
Pamoja na maelekezo hayo, Mkurugenzi Shauri aliwaasa Wakuu hao wa Shule kusimamia ujenzi wa madarasa hayo kwa uadilifu mkubwa na kuhakikisha hawamuangushi Rais Samia.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.