Wakandarasi wanaotekeleza Miradi mbalimbali ya maendeleo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na kukamilisha miradi kwa wakati kwa kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango na ufanisi unaotakiwa ili kuendana na thamani ya fedha.
Hayo yamebaibishwa leo Agosti 24, 2024 na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelya wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Jiji hilo.
Akiwa kwenye ziara hiyo, Mkurugenzi Mabelya ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ina lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati hivyo kutoa wito kwa wakandarasi wote kuhakikisha wanakamilisha miradi kwa wakati huku akiwataka wataalamu kutoka Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanafuatilia miradi hiyo kwa ukaribu zaidi.
“Nimetembelea miradi minne ya Afya pamoja na elimu kukagua lakini pia kubaini changamoto za miradi hiyo ilo kuweza kuzitatua na kazi iendelee kwani kupitia miradi hii tunaamini wanannchi wetu wataendelea kupata huduma stahiki kwa wakati hivyo niwaagize wakandarasi wote ambao wamesimama kuendelea na utekelezaji kwa sababu mbalimbali warudi kazini kuanza utekelezaji ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati uliopangwa, pia nipende kuwasisitiza wataalamu kutoka ofisi yangu kuhakikisha wanafuatilia miradi hiyo kwa ukaribu zaidi kwani nia yetu ni madhubuti kabisa ya kuhakikiaha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati zaidi”. Ameeleza Ndg. Mabelya.
Sambamba na hilo, amewasisitiza Wakandarasi hao kushirikiana na wataalamu kutoka ofisi yake pindi kukiwa na changamoto zozote wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo lengo likiwa ni kutatua changamoto hizo ili miradi itekelezwe na kukamilika kwa wakati na kwa viwango bora.
Akiongea kwa niaba ya Mkandarasi Humphrey Construction ambaye anatekeleza mradi wa Kituo cha Afya Mchikichini Mhandisi amemuhakikishia Mkurugenzi wa Jiji la Dar ea Salaam kuwa Agosti 26, 2024 mafundi wataendelea na kazi ya ujenzi na mradi utakamilika kwa wakati uliopangwa.
Aidha, miradi iliyotembelewa ni pamoja na Ujenzi wa Kituo cha Afya Mchikichini, ujenzi wa Maktaba na UkumbiShule ya Sekondari Benjamini Mkapa, Ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa nyasi bandia Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa pamoja na kukagua maendeleo ya mradi wa Machinjio ya Vingunguti ambapo miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.