Na;Rosetha Gange
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mhe.Amosi makalla leo tarehe 8/7/2021 amefanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Machinjio ya kisasa ya Vingunguti na kutoa agizo kwa Mkandarasi wa machinjio hayo ambaye ni Shirika la nyumba la Taifa (NHC) kuwa, mpaka kufikia tarehe 30/7 ujenzi uwe umekamilika ili tarehe 1/8 ianze kutumika rasmi.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa Machinjio hayo Mkurugenzi wa jiji la Dar es salaam Ndg.Jumanne Shauri amesema kuwa Halmashauri ya jiji la Dar es salaam ilisaini mkataba wa ujenzi wa Machinjio hayo na Shirika la nyumba la Taifa kwa gharama ya Sh.12.4Bil ambapo Sh.8.5 ni fedha kutoka Serikali kuu na Sh.3.9Bil ni mchango wa Halmashauri kutoka katika mapato yake ya ndani.
Aidha Ndg.Shauri amesema kwamba mpaka sasa Mkandarasi wa Machinjio hayo amekwishalipwa kiasi cha Sh.Bil 9 hivyo kubakiwa na deni la Sh.Bil.3.3.Mpaka sasa ujenzi wa Machinjio hayo umekwisha kamilika kwa 96% na wamejiwekea mpaka kufikia tarehe 1/8/2021 Machinjio hiyo ianze kutumika baada ya kukamilisha vitu vichache vilivyosalia kama ujenzi wa mabucha ya kuuzia nyama,kukamilisha ujenzi wa tanki la maji,kujenga banda la kuhifadhia ngozi pamoja na ujenzi wa chumba cha kuhifadhia baridi (cold room).
Akisisitiza kauli ya Kazi iendelee ya Mh.Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan,Mhe.Makalla amesema kuwa mradi wa machinjio hayo ni mkubwa na muhimu sana kwa nchi yetu hivyo ni lazima uanze kufanya kazi haraka ili serikali iweze kujipatia mapato na matarajio yaliyolengwa na Serikali yaweze kutimia.
Mhe Makalla anasema,
“Mradi huu unakwenda kubadilisha maisha na uchumi wa watu.Pia ni mradi ambao unakwenda kufungua fursa nzuri kwa mikoa mingine kwa sababu Dar es salaam inategemewa sana katika soko la mifugo.Vilevile mradi huu utatoa fursa kwa wafanyabiashara kupeleka nyama maeneo mengine kama Zanzibar,Comoro na Dubai.Hivyo Mkandarasi fanya kazi usiku na mchana kukamilisha kazi iliyobaki.”
Katika ziara ya ukaguzi wa Machinjio hayo Mhe.Makalla aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe.Ng’wilabuzu Ludigija,Meya wa Jiji la Dar es salaam Mhe.Omary Kumbilamoto,Mkurugenzi wa jiji la Dar es salaam Ndg.Jumanne Shauri na watendaji mbalimbali kutoka Halmashauri ya jiji la Dar es salaam.
Mradi wa Machinjio ya kisasa ya Vingunguti ulianza rasmi tarehe 8 Julai 2019 ukiwa unatekelezwa na Mkandarasi ambaye ni Shirika la nyumba la Taifa (NHC) akisimamiwa na Mshauri Mwenezi M/S CONS AFRIKA Ltd na FB Consultant wa Dar es salaam.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.