Katika kuhakikisha mkakati wa miaka 10 wa matumizi ya nishati safi ya kupikia unatekelezwa kwa ufanisi Mkuu wa Mkoa wa Dae es Salaam Mhe. Albert Chalamila ameendelea kushirikiana nawadau mbalimbali katika kufanikisha agenda hiyo kwa wananchi huku akiwasisitiza Wananchi wa Mkoa huo matumizi ya Nishati safi ya kupikia na kuacha matumizi ya nishati chafu.
Mhe. Chalamila ameyabainisha hayo wakati akipokea zaidi ya mitungi 800 ya gesi kutoka Kampuni ya Puma Energy Tanzania iliyofanyika katika viwanja vya Biafra - Kinondoni, Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Chalamila amesema Dar es Salaam ni kinara wa matumizi ya nishati chafu, hivyo uamuzi wa kugawa mitungi hiyo itasaidia kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kusisitiza kuwa kupika kwa gesi ni nafuu ukilinganisha na kuni au mkaa.
“Dar es salaam ndio mkoa unaotumia nishati chafu kutokana na wingi wa watu wanaotumia kuni na mkaa kwa ajili ya kupika hivyo uamuzi huu wa Puma Energy Tanzania unakwenda kumaliza au kupunguza matumizi ya nishati chafu katika mkoa wetu na Tanzania kwa ujumla hivyo nitoe wito kwa mama lishe na baba lishe wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha mnaibeba ajenda hii na kuachana na matumizi ya mkaa na kuni kwa kulinda mazingira lakini pia afya zenu kwa ujumla." Ameeleza Mhe. Chalamila.
Katika hatua nyingine, Mhe. Chalamila ameeleza uwepo wa Tamasha la Mapishi kwa kutumia Nishati safi siku ya Jumamosi, Novemba 2, 2024 katika Viwanja vya Biafra-Kinondoni pamoja na kuwaagiza Wakuu wa Wilaya za Temeke, Ilala, Kinondoni na Ubungo kushirikiana kuratibu siku ya Tamasha hilo ambalo litaambatana na 'Jogging club' itakayoanzia Magomeni mpka Biafra, itakayoambatana na ukaribisho wa makampuni ya vinywaji kama TBL, SBL, KONYAGI, PEPSI na COCA COLA kuja kuunga mkono na kujumuika katika Tamasha hilo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania Bi. Fatma Abdallah amesema kampuni hiyo imedhamiria kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na ndio maana wametoa mitungi hiyo ambayo itagawanywa kwa mama lishe na babalishe wa Wilaya zote tano za Mkoa wa Dar es Salaam.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.