Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila leo Mei 29, 2024 amefanya amefanya mkutano wa hadhara katika Jimbo la Ilala wenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Jimbo hilo.
Akiongea na wananchi kwenye mkutano huo, Mhe. Chalamila amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii Ili kujinasua katika wimbi la umaskini kwa maendeleo binafsi na Taifa kwa ujumla.
"Maendeleo hayaji kwa kulalamika. Maendeleo yanakuja kwa kufanya kazi kwa bidii, kujituma, malalamiko ni adui wa maendeleo. Changamoto ni nyingi katika jamii lakini tuzitumie changamoto kama fursa ya kujitengenezea vipato kwa maendeleo binafsi na Taifa kwa ujumla. Serikali ina mchango mkubwa kwenye maendeleo kwa kuboresha miundombinu, Elimu na sekta ya Afya hivyo na sisi tutumie maendeleo hayo kujitengenezea kipato na kujitoa kwenye umaskini”. Amesema Mhe. Chalamila
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amesema "Kipekee namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha katika Wilaya yetu, Nikuhakikishie kuzitumia fedha hizo kama zilivyokusudiwa kwa maendeleo ya Taifa , pia mafanikio haya tunayoyapata ni pamoja na maelekezo yako unayotupa, na nikuhakikishie kuwa tutaendelea kuimarisha mapato ya Halmashauri ya Jiji, na tupo tayari kupokea maagizo yako na kuyatekeleza.”
Aidha, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ilala Said Side amemuomba Mkuu Mkoa a kuboresha makazi ya wananchi wa Ilala Kota kwa kujenga maghorofa ili wakazi hao waishi katika mazingira mazuri .
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la DSM Mhe. Omary Kumbilamoto amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilala kwa juhudi anazozifanya katika kuhakikisha jimbo lake linapata maendeleo katika nyanja zote.
Akijibu kero ya maeneo ya kufanyia masoko, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Jomaary Satura amesema kuwa wanapambana kuhakikisha masoko mawili yatayojengwa (soko la mchikichini na soko la mbuyuni) yanakamilika kwa wakati na wafanyabiashara watapata maeneo ya kufanyia biashara zao bila bugudha.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.