Katika kuhakikisha mkakati wa miaka 10 wa matumizi ya nishati safi ya kupikia unatekelezwa kwa ufanisi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila Leo Septemba 12, 2024 amezindua kongamano la matumizi ya Nishati Safi ya kupikia katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam ambalo limehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Mameya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Watendaji Wakuu wa Taasisi ambata za Nishati safi, Viongozi wa dini na mamia ya mama lishe na baba lishe.
Akizindua kongamano hilo, RC Chalamila ameishukuru kampuni ya Lake Gas kwa kutoa mitungi 1000 ya Nishati safi kwa kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuachana na matumizi ya Nishati chafu badala yake kutumia Nishati safi ya kupikia.
"Niwaombe Taasisi, Mashirika na wadau wengine ndani ya Mkoa kuiga mfano wa kampuni ya Lake Gas kuendelea kutoa mitungi zaidi ya gesi ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi." Amesema RC Chalamila.
Aidha, Mhe. Chalamila ameongeza kuwa “Leo tumezindua kongamano la matumizi ya Nishati safi ya kupikia katika Mkoa wetu, kampeni hii ni endelevu tukiwa na lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kwenda sambamba na kaulimbiu ya 'Jali Afya, Pika Kijanja, Tumia Nishati Safi Okoa Mazingira Kwa Ukuaji wa Uchumi’ ambapo katika kuendelea kutekeleza hili tumeandaa tamasha kubwa la mapishi linalotarajiwa kufanyika Septemba 23, 2024 hivyo nitoe wito kwa Mama lishe na baba lishe na wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kongamano hilo".
Sambamba na hilo, RC Chalamila amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuratibu upatikanaji wa mitungi ya gesi kutoka Taasisi mbalimbali za serikali kuchangia mitungi kuanzia 200 hadi 300 kabla ya Septemba 30, 2024.
Aidha mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, ulizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Mei 8, 2024 ukilenga kuepuka athari za matumizi ya kuni na mkaa.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.