HALMASHAURI ya Wilaya ya Msalala imekuwa ya kwanza Kitaifa katika ukusanyaji wa mapato kwa kukusanya asilimia hamsini na mbili (52%) ya makisio ya mapato ya ndani kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/20 huku Halmashauri ya Kyerwa ikiwa ya mwisho kwa kukusanya asilimi tatu tu ya makisio yake.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo alipokuwa akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha Julai – Septemba, 2019.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imefanikiwa kukusanya mara mbili ya malengo ya robo ya kwanza ambapo kila Halmashauri inatakiwa kukusanya si chini ya asilimia 25 ya makisio ili kukamilisha asilimia 100 kwa robo nne za mwaka wa fedha.
Waziri Jafo alieleza kuwa Bajeti iliyoidhinishwa ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2019/20 ni shilingi Bilioni 765.48; Katika kipindi cha robo ya kwanza (Julai hadi Septemba, 2019) Halmashauri zimekusanya jumla ya shilingi bilioni 166.24 sawa na asilimia 22 ya makisio ya mwaka.
Alifafanua kuwa “Katika kipindi hiki Halmashauri zilipaswa kukusanya asilimia 25 ya makisio yake ya mwaka lakini Halmashauri hamsini na nne tu (54) ndio zilizofanya vizuri kwa kukusanya zaidi ya asilimia 25 ya bajeti zao na Halmashauri 121 hazikuweza kufikisha asilimia 25 ya mapato yake”.
Aidha, Mhe. Jafo alisema kuwa katika kuzipima Halmashauri zote kwa pamoja Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya shilingi Bilioni 13.10 na Halmashauri ya Buhigwe imekuwa ya mwisho kwa kukusanya shilingi Milioni 35.15.
Pia Mhe. Jafo aliongeza kuwa katika ngazi ya Mikoa, Mkoa wa Rukwa umeongoza kwa kukusanya wastani wa asilimia thethini na moja (31) ya makisio ya Halmashauri za Mkoa huo huku Mkoa wa Mwisho ukiwa ni Mtwara ambao Halmashauri zake zimekusanya wastani wa asilimi kumi na tatu (13) ya makisio yake.
Alisema Katika kipengele hicho cha Mikoa kwa kuzingatia wingi wa mapato Mkoa ambao unaongoza kwa kukusanya mapato ya ndani kwa wingi ni Mkoa wa Dar es Salaam ambao umekusanya shilingi Bilioni 39.53 na Mkoa wa Mwisho katika wingi wa ukusanyaji wa mapato ni Mkoa wa Kigoma ambao umekusanya shilingi bilioni 2.12.
Akisoma mchanganuo wa ukusanyaji wa mapato kwa kuzingatia aina ya Halmashauri na vigezo mbalimbali Mhe. Jafo amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeongoza kundi la Halmashauri za Majiji kwa kukusanya mapato kwa asilimia 38 ya makisio yake ya mwaka huku Halmashauri ya Jiji la Dodoma ikiwa ya mwisho katika kundi hili kwa kukusanya kwa asilimia kumi na nane (18%) ya makisio yake ya mwaka.
Mhe. Jafo alitaja Halmashauri za Majiji zilizokusanya mapato ya ndani kwa kigezo cha wingi (Ghafi) kuwa Jiji la Dodoma limeongoza kwa kukusanya shilingi bilioni 13.098 na Halmashauri ya Jiji la Mbeya imekuwa ya mwisho katika kundi hili kwa kukusanya shilingi bilioni 2.74 tu.
Hali kadhalika Jafo alitaja Manispaa iliyoongoza kundi la Halmashauri za Manispaa kwa kigezo cha asilimia kuwa ni Manispaa ya Sumbawanga ambayo imekusanya kwa asilimia arobaini na mbili (42) na Manispaa ya mwisho katika kigezo hiki ni Manispaa ya Kigoma ambayo imekusanya kwa asilimia tisa tu ya makisio yake kwa mwaka.
“Katika kigezo cha wingi wa mapato kundi hili linaongozwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ambayo imekusanya shilingi bilioni 13.05 huku Manispaa ya Kigoma ikiwa ya mwisho tena kwa kukusanya kiasi kidogo cha fedha cha shilingi milioni 235.11 alisema Jafo”.
Akifafanua kipengele cha Halmashauri za Miji Jafo alisema kuwa Mji wa Tunduma umeongoza kwa kukusanya kwa asilimia thethini na tisa (39%) na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekua ya mwisho kwa kukusanya asilimia nne (4%) ya makisio ya mapato yake ya ndani kwa mwaka.
Mhe. Jafo alisema kuwa Halmashauri ya Mji wa Geita imeendelea kuongoza kwa wingi wa mapato katika Halmashauri za Miji kwa kukusanya shilingi bilioni 2.34 na Halmashauri ya mwisho ni Mji wa Nanyamba ambayo imekusuanya shilingi milioni 74.72.
Wakati huo huo Jafo alizataja Halmashauri za Wilaya zilizofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato kiasilimia kuwa ni Halmashauri ya Msalala ambayo imekusanya kwa asilimia hamisni na mbili (52%) na Halmashauri ya Kyerwa imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia tatu (3%) ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka.
Upande wa wingi wa mapato Mhe. Jafo alitaja Halmashauri ya Wilaya iliyoongoza katika kundi hili kuwa ni Halmashauri ya Chalinze ambayo imekusanya shilingi bilioni 2.05 na ya mwisho ni Halmashauri ya Buhigwe iliyokusanya shilingi milioni thethini na tano (35) tu.
Jafo alisema kuwa katika matumizi ya mapato ya vyanzo vya ndani katika taarifa hii ya robo ya kwanza haionyeshi picha halisi ya uchangiaji wa mapato hayo katika shughuli za maendeleo kwenye sekta ya Elimu, Afya na Maji.
“Uchambuzi kamili wa uchangiaji wa kila Halmashauri katika miradi ya maendeleo utafanyika katika robo ya pili na mwisho wa mwaka wa fedha 2019/20 lakini kila Halmashauri ifanye jitihada kuhakikisha inachangia mapato ya ndani kulingana na asilimia inayopaswa kuchangiwa kwa mujibu wa bajeti zake” Alifafanua Jafo.
Aidha, Mhe. Jafo alieleza kuwa katika kipindi cha Julai-Septemba, 2019 Halmashauri zilitumia shilingi Bilioni 40.88 kati ya shilingi bilioni 340.68 zilizokasimiwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo sawa na asilimia 12.
Mhe. Jafo alikumbushia matumizi sahihi ya Mifumo ya Kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato na mashine za kukusanyia mapato (PoS’s) na mifumo ya Kielektroniki ya kutolea taarifa.
Alimalizia kuwataka viongozi kuweka mikakati madhubuti ya kukusanya mapato kutoka kwenye vyanzo vipya vinavyobuniwa na Halmashauri zao.
(mwisho).
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.