HOTUBA YA MGENI RASMI MHE.SAMIA SULUHU HASSAN MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ILIYOSOMWA NA NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO MHE. HAMIS ANDREA KIGWANGALA
KATIKA KILELE CHA SHEREHE ZA MAONESHO YA WAKULIMA, WAFUGAJI NA WAVUVI KANDA YA MASHARIKI KATIKA UWANJA WA MWL. J.K. NYERERE MKOA WA MOROGORO
TAREHE 08/08/2017
Mheshimiwa, Dkt. Kebwe S. Kebwe Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,
Waheshimiwa, Wakuu wa Mikoa ya Tanga, Pwani na Dar es Salaam,
Ndugu Makatibu Tawala Mikoa ya Morogoro, Tanga, Pwani, na Dar es Salaam
Mheshimiwa, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro,
Mheshimiwa, Innocent Karogeles,
Ndugu, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro Bw. Kurwa Omari Milonge
Wakuu wa Wilaya wote Kanda ya Mashariki,
Waheshimiwa Wabunge wote mliopo,
Wastahiki, Mameya wa Kanda ya Mashariki mliopo,
Waheshimiwa, Wenyeviti wa Halmashauri mliopo,
Waheshimiwa Madiwani,
Waheshimiwa, Wawakilishi wa vyama rafiki
Wakuu wa Vyuo,
Wakurugenzi wote,
Wakuu wa Taasisi na Mashirika mbalimbali
Wadau wa Maendeleo
Wakulima, Wafugaji na Wavuvi wote
Ndugu Washiriki wote wa Maonesho,
Wanahabari,
Wageni waalikwa
Mabibi na Mabwana.
Ndugu Viongozi, Washiriki na Wananchi,
Awali ya yote namna kumshukuru Mungu kwa kutujalia Afya njema kwa kutuwezesha kukutana hapa leo.
Pili, nawashukuru waandaaji, washiriki na waoneshaji wa sherehe hizi za Wakulima, Wafugaji na Wavuvi.
Tatu, kwa namna ya pekee, nawashukuru Viongozi wa Kanda ya Mashariki kwa kunipa heshima hii kubwa ya kuwa mgeni rasmi kwenye siku hii ya kilele cha sikukuu ya wakulima, wafugaji na wavuvi; maarufu kama Nanenane zinazofanyika Kikanda hapa Morogoro.
Ndugu Viongozi, Washiriki na Wananchi,
Maonesho ya Kilimo katika Uwanja huu wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere yamefana sana na yanazidi kuvutia wadau wengi mwaka hadi mwaka. Hali hiyo nimeiona, baada ya kutembelea mabanda na mashamba ya vipando vilivyoandaliwa ambapo inathibitisha kwamba juhudi za dhati zimefanyika katika maandalizi ya Maonesho na pia katika kuendeleza Uwanja huu.
Aidha, inaonesha kwamba Wadau wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wanazidi kutambua umuhimu wa Maonesho ya Nane Nane kama njia mojawapo ya kuwaenzi wakulima, wafugaji na wavuvi kwa kutambua mchango wao katika uchumi wa Taifa letu kama inavyobainishwa kwenye kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “ZALISHA KWA TIJA MAZAO NA BIDHAA ZA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI ILI KUFIKIA UCHUMI WA KATI “.
Ndugu Wananchi,
Nawapongeza washiriki wote kwa kujenga na wanaoendelea kujenga majengo mazuri na ya kudumu. Serikali kwa kutambua juhudi zenu, mapema kabisa iliuteua Uwanja huu kuwa wa Kitaifa kwa Maonesho ya Kilimo tangu mwaka 2004. Aidha, tangu Serikali iuteue Uwanja huu kuwa wa Kitaifa mwaka 2004 nimeambiwa kuwa juhudi za makusudi zimekuwa zikifanywa na viongozi wa Mikoa ya Kanda kuboresha uwanja huu ili kufikia hadhi ya Kitaifa.
Natoa wito kwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mikoa ya kanda ya Mashariki, Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, wadau wa maendeleo na washiriki kwa jumla kuanzia sasa kuchukua hatua za makusudi kuimarisha Uwanja huu hasa baada ya TASO kufutiwa usajili na shughuli za uratibu kuletwa katika Sekrtarieti za Mikoa. Kufanya hivyo kutaufanya uwanja huu uwe kivutio hata kwa wadau wengine ndani ya nchi na hata kutoka nje hususani nchi za Afrika Mashariki, kushiriki na kuwekeza katika uwanja huu.
Ndugu Wananchi,
Katika kutembelea mabanda mbalimbali kwa mujibu wa ratiba niliyokuwa nimepangiwa, nimeona teknolojia mbalimbali zinazoweza kutumiwa na Wakulima Wafugaji na Wavuvi wetu katika kuongeza uzalishaji bora wenye tija, ili kufikia azma ya nchi yetu ya kufikia uchumi wa kati mwaka 2025.
Nimepata fursa ya kuzungumza na Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika, Wataalam, Wafanyabiashara wa mazao, pembejeo na zana za kilimo, wote wanayo ari kubwa ya kushiriki katika kuleta MAPINDUZI katika Sekta hizo.
Ndugu Wananchi,
Kwa kuzingatia ujumbe wa mwaka huu wa kuzalisha kwa tija Wakulima, Wafugaji na Wavuvi wanaweza kuleta mapinduzi makubwa katika kilimo, ufugaji uvuvi na hifadhi ya mazingira kama yafuatayo yatazingatiwa:-
Ndugu Wananchi,
Kama yaliyotajwa hapo juu tutayazingatia, mazingira yetu yataboreshwa na umaskini kwa wananchi wetu utapungua kwa kujiongezea kipato. Uchumi wa Taifa letu kwa ujumla utakua pia.
Ndugu Wananchi,
Kama inavyoeleweka Maonesho ya Kilimo ni njia mojawapo ya kuelimisha Wakulima, Wafugaji na Wavuvi. Katika Maonesho ya mwaka huu kuna baadhi ya Waoneshaji wanaotoa elimu ya kuongeza ubora wa mazao yetu na kuhifadhi kwa njia mbalimbali za kiasili na kisasa.
Aidha, taaluma hii ni muhimu katika kupunguza kiwango cha upotevu wa mazao yanayoharibika, wakati na baada ya kuvuna. Njia hizi ni muhimu ili kuongeza ubora wa mazao na muda wa kukaa bila kuharibika kwa kuoza au kushambuliwa na wadudu.
Usindikaji wa mazao, kama njia ya kuyaongeza thamani, ni hifadhi nzuri inayompatia mkulima, mfugaji na mvuvi muda wa kutafuta masoko, ili hatimaye kuuza kwa bei nzuri.
Ndugu Wananchi,
Wafugaji wengi hapa Tanzania ni wachungaji, hawapati faida ipasavyo kutokana na mifugo yao kwa sababu mavuno yanayotokana na mifugo hiyo ni duni sana, hivyo kupata bei za chini mno katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Kwa ujumla mifugo waliyonayo wafugaji haina tija.
Inabidi kubadilika kutoka uchungaji na kuwa wafugaji wa mifugo, ili mfugaji afaidike na mifugo yake hana budi kuwa na shamba la mifugo lililopimwa, ili aweze kuendeleza malisho ndani yake, na kudhibiti magonjwa. Kwa kufanya hivyo mazao ya mifugo kama nyama, ngozi na maziwa yatapata soko zuri ndani na nje ya nchi kama ambavyo tumeona katika mabanda mengi ya mifugo.
Ndugu Wananchi,
Mkulima hawezi kupunguza umaskini kwa kilimo bora na ufugaji bora tu, bila ya kuwa na chombo kama ushirika, kumsaidia kujua masoko, kupata mikopo n.k mkulima mmoja mmoja, hawezi kumudu gharama za kutafuta masoko au kukidhi masharti ya Mabenki kupata mikopo. Wakulima ni lazima wajiunge katika vikundi vya ushirika vya uzalishaji na SACCOS, ili kuweza kupata mikopo yenye riba nafuu, kwa urahisi. Aidha, elimu ya ushirika inayotolewa kwenye Maonesho ya mwaka huu, iwe changamoto kwenu kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Ndugu Wananchi,
Ingawa Maonesho haya ya kilimo yamefanyika kikanda, ni imani yangu kwamba, wakulima, wafugaji na wanaushirika waliopata nafasi ya kutembelea Uwanja, na kuona Maonesho, au kushirikiri katika kuonesha kwa njia moja au nyingine, wameweza kupata teknolojia mpya, kujifunza mbinu mpya za uzalishaji, kujua masoko ya mazao yao na jinsi ya kuyasindika na kuyahifadhi.
Aidha, Wakulima wamepata nafasi ya kujua teknolojia mpya, na zana mbalimbali, na jinsi ya kuzitumia. Nina imani kwamba elimu na maarifa waliyoyapata katika Maonesho haya, watayatumia katika shughuli zao za uzalishaji na kufundisha wenzao, ambao hawakupata nafasi ya kufika hapa. Vyombo vya habari vimesaidia kwa kiasi kikubwa kufikisha elimu na maarifa kwa wananchi wote kupitia vyombo vyao nawapongeza na kuwataka waendelee kwa kuandika Makala mbalimbali na kuwafikishia wananchi.
Ndugu Wananchi
Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wetu Mhe Dr John Pombe Joseph Magufuli, inalenga kujenga uchumi wa viwanda. Ili kufikia malengo hayo ni lazima kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo ambayo ndiyo yatakuwa mali ghafi katika viwanda vinavyotarajiwa kujengwa. Tunahitaji kuongeza thamani ya mazao yetu ya kilimo na mifugo ili yawweze kupata soko zuri ndani na nje ya nchi. Uchakataji wa mazao kupia viwanda ndiyo njia sahihi ya kuongeza thamani ya mazao hayo na hivyo kuongeza mapato ya wakulima wetu na taifa kwa ujumla.
Ndugu Wananchi,
Kabla ya kutangaza kufunga maonesho haya, nachukua fursa hii tena kuwashukuru Mhe. Dkt. Kebwe S. Kebwe, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martin Shigela Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Paul Makonda Mkuu wa Dar es Salaam, Mhe. Eng. Evarist Ndikilo Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Pia nichukue fursa hii kukupongeza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kuisimamia vyema Kamati ya Uratibu ya Maonesho ya Nanenane inayoundwa na Sekretairieti za mikoa hii mine ya kanda ya Mashariki, iliyofanya kazi nzuri ya maandalizi badala ya kufutwa kwa TASO. Kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Morogoro chini ya Mhe. Regina Chonjo Mkuu wa Wilaya, Wakuu wa Wilaya wote, Mameya na Wenyeviti wa mamlaka ya Serikali za Mitaa na Wakurugenzi Kanda ya Mashariki, Wanahabari Washiriki wote wa Maonesho katika Uwanja wa Mwl. J.K. Nyerere kwa juhudi mlizofanya kufanikisha Maonesho haya.
Baada ya kusema hayo, sasa natangaza rasmi kuwa Maonesho ya Nanenane mwaka 2017 Kanda ya Mashariki yamefikia kilele.
Asanteni kwa kunisikiliza.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.