Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amemtaka Mkandarasi anayejenga Kituo Kikuu cha Mabasi cha Mbezi Luis, ‘Hainan International Limited' kuhakikisha ifikapo tarehe 30 Novemba, 2020 ujenzi wa kituo hicho uwe umekamilika.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 08 Oktoba, 2020 jijini Dar es Salaam kabla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo Kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Mbezi Luis kwa pamoja na mgeni wake rais wa Malawi Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera.
Amesema kuwa iwapo Mkandarasi huyo atachelewa kufanya hivyo atapaswa kukatwa fedha kwa kuwa hakuna sababu ya msingi inayozuia ukamilishwaji wa mradi huo kwa wakati.
Mheshimiwa Rais Magufuli ameagiza ndani ya kituo hicho cha mabasi kuwepo na ofisi ya Uhamiaji kwa kuwa kitakuwa na mabasi yanayoingia na kutoka nchi jirani na pia uwekwe mgawanyo mzuri wa maeneo ya maegesho ya magari ikiwa ni pamoja na kutenga eneo la mabasi yaendayo nje ya nchi, mabasi yaendayo mikoani, teksi, bodaboda na bajaj.
“Nimeambiwa hapa pakikamilika patakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi ya abiria 1,000, teksi 280 kwa siku, patakuwa na maeneo ya bodaboda na bajaji na patakuwa na eneo la mamalishe na babalishe”, Alifafanua Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa amefurahishwa kushuhudia utekelezaji wa mradi huo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 85 na kueleza kuwa ni “MATOKEO CHANYA ya miradi inayotelezwa na Serikali.
Awali akizungumza katika tukio hilo Rais wa Malawi, Dkt. Chikwera alisema kuwa Tanzania imeonyesha mfano kwa kutekeleza mradi kwa kutumia fedha zake na kubainisha kuwa ujenzi wa stendi hiyo utaboresha mahusiano ya kibiashara yanayofanywa baina ya nchi hizo mbili na za ukanda wa SADC kwa ujumla.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.