Na. Judith Damas
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amezindua mkakati endelevu wa Usafi na uhifadhi wa mazingira Dar es salaam ambapo ameelekeza kila Mtendaji kusimamia Usafi na kuhakikisha sheria inatumika kutoa adhabu kwa wachafuzi wa mazingira, hayo ameyabainisha leo Novemba, 23 katika mkutano wa Uzinduzi wa Usafi na uhifadhi wa Mazingira Dar es Salaam wenye kauli mbiu isemayo 'Safisha Pendezesha Dar es Salaam' uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, ukiwa umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa kiserikali, Chama Cha Mapinduzi, Viongozi wa Dini, Wastahiki Meya, Vyombo vya ulinzi na usalama, Maafisa Mazingira, Wenyeviti na Watendaji wa Mitaa na wadau mbalimbali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Makalla ametoa maelekezo 10 kwa Viongozi wote na wananchi wazingatie ili kufanikisha Kampeni hiyo ikiwemo Kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuwa siku ya Usafi wa pamoja "Kila Manispaa iteue wakandarasi wa Usafi Wenye Sifa na Vigezo, ikiwemo Vifaa vya kutosha vya kufanyia Usafi, Kila Manispaa kupitia upya Sheria za udhibiti wa Biashara holela na Usafi na Kama hazipo zitungwe, Kila Mwenyekiti na Mtendaji wa Mtaa kuhamasisha na kusimamia Usafi kwenye eneo lake, Mkataba na kila Manispaa kusimamia Usafi na Machinga wasirudi kwenye maeneo yaliyokatazwa, kila Taasisi kulinda maeneo yake ili yasivamiwe na Machinga, Wakuu wa Wilaya kusimamia Usafi katika maeneo ya fukwe zote za Mkoa huo kufanyiwa Usafi na uwe endelevu, Amepiga marufuku tabia ya Wizi wa vyuma na minyororo iliyowekwa kwaajili ya kupendezesha mandhari ya Jiji(vigingi) pia ameeleza kuwa usafi unaendana na muonekano mzuri wa majengo hivyo ameelekeza majengo yote yapakwe rangi yawe na muonekano mzuri.
Sambamba na hayo Mhe. Makalla ametoa wito kwa Wananchi kuitumia siku ya tarehe 4 Desemba ambayo ndiyo siku ya uzinduzi wa Usafi Kata ya Kivukoni kwa kufanya Usafi wa kina kwenye maeneo yao ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Sherehe za Uhuru.
Kwa upande Mwingine Mhe. Makalla ameweza kuingia mkataba na Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wote wa Kila Halmashauri kusimamia usafi na Kuhakikisha Wafanya biashara ndogondogo hawarudi tena katika maeneo yasiyo rasmi na maeneo hayo yafanyiwe usafi wa kina.
"Mkataba huu ulioambatana na mahudhurio kama makubaliano ya kutekeleza suala zima la usafi na uhifadhi wa mazingira utasainiwa na Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi wa kila Halmashauri na mkitoka hapa mhakikishe mnapitia sheria ndogondogo za usafi na kama hazipo mkazitunge, muende mkajifunze kwa wenzenu waliwezaje kufanikisha suala zima la usafi Katika Mikoa yao." Ameeleza Mhe. Makalla.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa DSM Bi. Cathe Kamba amempongeza Mkuu wa Mkoa wa DSM pamoja na Viongozi wake kwa kazi nzuri walioifanya ya kuwapanga wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Machinga kutoka sehemu zisizo rasmi na kwenda kufanya biashara maeneo rasmi hivyo ameahidi kushirikiana na viongozi hao katika kampeni ya usafi na uhifadhi wa mazingira Mkoa wa Dar es Salaam na kuhakikisha Mkoa unakua safi.
Akitoa shukrani zake Kwa Mkuu wa Mkoa Mwenyekiti wa Machinga Bw. Masoud Issa amesema" Tunamshukuru Mkoa wa Mkoa Mhe. Makalla kwa kutushirikisha katika zoezi zima la kutupanga katika maeneo rasmi na kwaniaba ya Wamachinga wenzangu naahidi hatutomuangusha tutabaki katika maeneo rasmi na tutahakikisha tunafanya usafi na tunahifadhi mazingira ili kuipendezesha Dar es Salaam."
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.