Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul C. Makonda leo tarehe 09 Septemba, 2017 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa viwanda vidogo vidogo vinavyojengwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika eneo la Mwananyamala jijini Dar es Salaam ili kuwawezesha wajasiriamali kuboresha ustawi wa maisha yao.
Akiongea katika hafla hiyo Mhe. Makonda ametoa pongezi kwa Waheshimiwa Madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kujenga na kuboresha mazingira rafiki kwa lengo la kuchochea maendeleo kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imetaja utaratibu wa kuweka asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya Wanawake, Vijana na Walemavu na kuagiza kwamba Manispaa za Jiji la Dar es Salaam ziige mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliyoanza ujenzi wa miundombinu rafiki kwa wanufaika wa mikopo kwa kuhakikisha kwamba inawajengea miundombinu wanufaika wa mikopo ya Halmashauri katika kila Manispaa za Jiji la Dar es Salaam.
Mhe Makonda amesema mfumo wa sasa hauna utambuzi wa kutosha kwa vijana, wanawake na walemavu kutokana na makundi hayo kutawanyika kibiashara jambo linalosababisha changamoto ya ufuatiliaji wa mikopo hiyo, na kuziagiza Manispaa za Jiji la Dar es Salaam kutenga maeneo maalum ya uanzishaji wa VIWANDA VIDOGO VIDOGO kwa ajili ya makundi hayo, hatua itakayowaweka pamoja na hivyo kutoa fursa kwa Serikali ya Mkoa kuwahudumia vizuri hususan katika kuwawezesha kupata mafunzo ya kuwaongezea ujuzi na utaalamu, masoko na pia kuwaunganisha na Wafanyabiashara wakubwa.
Awali akiwasilisha taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Sipora Liana alimweleza Mhe. Paul Makonda kuwa ujenzi wa viwanda hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa Kauli Mbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli, inayochochea uanzishwaji wa viwanda nchini kufikia malengo ya uchumi wa kati ambapo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, pamoja na kuwawezesha wawekezaji wakubwa wa viwanda kufikia malengo yao na kuwajengea mazingira bora ya uwekezaji, imepanga kujenga viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya akina mama, vijana na walemavu wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na kuwapatia fedha za mikopo zinayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
"Katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilitenga kiasi cha shilingi 200,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo vidogo ambao utekelezaji wake ulianza tarehe 01 Juni, 2017 ambapo hadi kufikia mwezi Agosti, 2017 ujenzi wa miundombinu hiyo umefikia asilimia 95. Gharama za mradi huo ni shilingi 199,988,052.00. Ujenzi huo utaendelea kutekelezwa na Halmashauri ya Jiji katika Manispaa za Ilala, Kigamboni, Temeke na Ubungo kwa kadri maeneo yatakavyopatikana", alieleza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo inashirikiana na Shirika la Kukuza Viwanda Vidogo Vidogo(SIDO) kuwajengea uwezo wajasiriamali hao itawawezesha kupata mafunzo yatakayowasaidia kuboresha zaidi uzalishaji na biashara zao. Kwa upande mwingine itakuwa rahisi zaidi kwao kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha, wadau mbalimbali pamoja na huduma muhimu kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA) na wadau wengine.
Kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi, tovuti ya Halmashauri pamoja na mitandao ya kijami, Halmashauri ya Jiji itawasaidia wajasiriamali hao kujitangaza zaidi ili waweze kupata masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi na inatoa wito kwa wajasiriamali wote watakaopata nafasi katika viwanda hivyo kuitunza miundombinu katika maeneo yote yatakayojengwa viwanda hivyo kwa maslahi ya wananchi wote.
Bonyeza hapa kuangalia picha zaidi za tukio hilo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.