Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda ameeleza kwamba matumizi ya rasilimali za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yatakua ni mwarobaini wa kutatua kero na malalamiko mbalimbali ya wananchi jijini Dar es Salaam.
Makonda ameeleza hayo leo, Oktoba 9, 2019 katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam wakati akizindua Mfumo wa kupokea na kushughulikia kero na malalamiko ya wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
RC Makonda aliendelea kueleza kwamba ameamua kuanzisha mfumo huo baada ya kubaini kuwa wananchi wengi jijini Dar es Salaam wanapoteza muda na gharama nyingi ili kuweza kufika katika ofisi za umma kuwasilisha malalamiko yao na katika ufuatiliaji wa malalamiko waliyowasilisha.
Aidha RC Makonda amebainisha kuwa mfumo huo utakuwa ukipokea taarifa za malalamiko ya wananchi na watumishi husika kuweza kuyafanyia kazi malalamiko yaliyowasilishwa kwa wakati, ikiwa ni pamoja na kuwezesha kufanya ufuatiliaji na kujua kila hatua iliyofikiwa tangu malalamiko yalipo sajiliwa mpaka ufumbuzi ulipopatikana na hivyo kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa watendaji katika ngazi zote.
“Mfumo huu unawawezesha viongozi kuona hatua mbalimbali za malalamiko kadri yanavyo fanyiwa kazi na kutoa ushauri ipasavyo ikiwa ni pamoja na kupata taarifa kwa nyakati tofauti tofauti kadri zitakavyo hitajika”, alieleza RC Makonda.
Hata hivyo RC Makonda amewahimiza wananchi kutumia mfumo huo unaopatikana kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu "SMS", Tovuti "Web address" na Mobile App na kuweza kuwasilisha malalamiko yao katika sekta tofauti tofauti ikiwemo Afya, Barabara, Elimu, Maji, Umeme na pia uwasilishaji wa taarifa za Miradi inayokwama pamoja na kutoa taarifa pindi wanapobaini uhalifu kwenye maeneo yao ya Mitaa.
Wananchi na wadau mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam wanaweza kuwasilisha malalamiko yao kwa kupitia ujumbe mfupi wa simu za mkoanoni kwa kuandika neno DSM 11000 kisha maelezo ya malalamiko/changamoto na kutuma kwenda namba 15200 au kwa kuingia kwenye tovuti kwa kupitia anuani; www.malalamiko.dsm.go.tz na ujumbe wao utapokelewa mara moja na kupewa namba ya lalamiko husika kwa ajili ya ufuatiiaji.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.