Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija, leo tarehe 19 Disemba, 2022 ameifungua rasmi stendi ya Daladala ya Kinyerezi iliyopo katika Kata ya Kinyerezi Mtaa wa Kibaga.
Mhe. Ludigija Amesema kuwa,stendi hiyo iliyojengwa chini ya mradi wa DMDP pamoja na kipande cha barabara ya lami cha Kilomita 7.1 na Madaraja ya Ulongoni A na B, na kugharimu kiasi Cha Jumla ya Shilingi Bilioni 17.5 vimerahisisha sana huduma za usafiri Kati ya Kata za Gongolamboto, Kinyerezi, Ukonga na maeneo jirani na kata hizo hivyo kuwaondolea wananchi adha ya mawasiliano waliyokuwa wanakumbana nayo.
Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa stendi hiyo ambayo siyo tu umerahisisha mawasiliano bali utaongeza Mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hivyo kupata Fedha itakayotumika kutekeleza miradi mingine ya Maendeleo mfano Ujenzi wa Vituo vya afya, shule, barabara na kuongeza ajira kwa wananchi wakiwemo Madereva wa Bodaboda, bajaji, mama na baba Lishe n.k.
Pia amewaomba wananchi kuitunza kikamilifu miradi inayotekelezwa na Serikali ili iweze kudumu vizazi hadi vizazi.
Amesema, "Ninawaomba wananchi mtumie vizuri matunda ya Rais wenu kwa kuwajengea stendi nzuri na ya kisasa ya Kinyerezi. Muitunze vizuri iweze kuwasaidia ninyi na vizazi vijavyo"
Sambamba na hayo Mhe. Ludigija ametoa maagizo kwa wafanyabiashara wote wanaofanya biashara maeneo yasiyo rasmi ikiwemo kando ya barabara, juu ya bomba la gesi na wale wenye mpango wa kwenda kufanya biashara katika stendi hiyo mpya, wote wametakiwa kwenda kufanya biashara zao katika soko la Kinyerezi maarufu Kama mnadani.
Naye Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto amempongeza Mkurugenzi wa Jiji kwa kufuata maagizo yote waliyoyatoa Jumamosi ya tarehe 17 Disemba 2022 walipofanya ziara ya kushtukiza katika stendi hiyo na kupelekea kazi ya ufunguzi wa stendi hiyo kufanikiwa kwa urahisi.
Mhe. Kumbilamoto pia amemuomba Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kusimamia Ulinzi na Usalama wa abiria katika stendi hiyo na kuhakikisha suala la Usafi linapewa kipaumbele ndani na nje ya stendi hiyo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.