Na: Shalua Mpanda
Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mheshimiwa Omary Kumbilamoto ametembelea na kufanya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Mzinga kilichopo kata ya Mzinga kujionea utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutaka miradi yote kukamilika kwa wakati.
Akiwa katika Kituo hicho, Meya Kumbilamoto amesema ujenzi wa kituo hicho kilichosimama kwa takribani miaka sita ni moja kati ya miradi inayoenda kwa kasi ili kukamilisha ndani ya muda uliowekwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan, alitupa maelekezo tuhakikishe miradi yote viporo inakamilika inapofika mwezi wa tatu,maelekezo hayo tumeyatii na tunakwenda spidi sana kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati". Alisema Mhe. Kumbilamoto
Aidha, Mstahiki Meya huyo amempongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelya kwa kukamilisha miradi mingi ambayo ilikwama kutokana na changamoto mbalimbali.
Mkazi wa mtaa wa Magole Bw.Said Salehe 'Mahuta" ameipongeza Serikali kuendeleza ujenzi wa kituo hicho kitakachowawezesha kupunguza changamoto ya huduma za afya katika eneo hilo ambapo kwa sasa huduma hizo huzipata katika kata za jirani za Kivule na Kitunda.
Ujenzi wa kituo chenye hadhi ya hospitali kinatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu na kitaweza kuhudumia wakazi wa kata hiyo yenye idadi ya wakazi zaidi ya elfu 45.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.