Na: Doina Mwambagi
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Elihuruma Mabelya, leo Juni 23, 2025 wameungana na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutembelea eneo litakapojengwa Shule ya Mfano ya Benki ya CRDB (CRDB Bank Model School), shule ya ghorofa nne inayotarajiwa kuwa ya kisasa zaidi jijini Dar es Salaam.
Shule hiyo mpya ya sekondari itakuwa na madarasa 16, maabara za kisasa 4, vyoo vya kisasa, na ofisi bora za walimu, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuboresha mazingira ya ujifunzaji kupitia ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, amesisitiza dhamira ya serikali kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora na uwazi.
“Tutashirikiana kwa karibu na CRDB Benki kuhakikisha kuwa mradi huu unakamilika ipasavyo, kwa ubora unaostahili na kwa wakati uliopangwa. Serikali ya Wilaya itahakikisha kuwa thamani ya mradi huu inaendana kikamilifu na fedha zinazowekezwa,” ameeleza Mpogolo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Elihuruma Mabelya, ameeleza kuwa mradi huo ni zawadi kwa vizazi vijavyo na ni kielelezo cha ushirikiano mzuri kati ya sekta binafsi na serikali.
“Mradi huu wa shule ya mfano unaakisi dhamira ya kweli ya kuwekeza kwenye kizazi cha sasa kwa ajili ya Tanzania ya kesho. Tunapongeza CRDB na Mbunge wa Ilala kwa kujitoa na kushirikiana nasi katika kuinua sekta ya elimu,” alisema Mabelya.
Mkurugenzi Mabelya ameongeza kuwa hadi sasa Jiji lina jumla ya shule 118, na Shule ya Mfano ya CRDB itakuwa ya 119. Ameeleza kuwa kuna uhitaji mkubwa wa uwekezaji zaidi katika sekta ya elimu ili kufikia matokeo chanya, na kwamba mradi huo unakwenda sambamba na sera ya uwekezaji kwa jamii, hivyo Halmashauri inajivunia kuwa sehemu ya utekelezaji wake.
Mradi huu unakwenda sambamba na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwekeza kwa dhati katika sekta ya elimu kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.