Na: Doina Mwambagi
Mkurugenzi wa Halmashauri Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Elihuruma Mabelya amesema kuwa Jiji la Dar es Salaam litaendelea kuzingatia sheria na kanuni zote za utoaji wa mikopo ili kuhakikisha kuwa fedha zinazotolewa zinawanufaisha walengwa .
Hayo ameyasema Leo februari 24, 2025 wakati wa mkutano maalumu wa utambulisho wa benki katika usimamizi wa utoaji wa mikopo halmashauri ya jiji uliofanyika katika ukumbi wa Anartoglou Jijini humo.
Mkurugenzi Mabelya ameeleza kuwa mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi kwa kuwapa fursa ya kujiajiri pamoja na kukuza biashara zao.
“Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kushirikiana na benki za CRDB na NMB, tumejipanga kuhakikisha kwamba mikopo inatolewa kwa kufuata kanuni na taratibu ili iwafikie walengwa sahihi. Hatutabaki kwenye maneno pekee, bali tumejizatiti kutekeleza hili kwa vitendo. Hadi kufikia Februari 12, tumepokea jumla ya maombi 945, na kwa sasa tuko katika hatua ya kuyachambua kwa kina ili kuhakikisha kila anayestahili anapata fursa hii .” Amesisitiza Mabelya
Sambamba na hilo, Ndugu Mabelya amesema kuwa Halmashauri itahakikisha inafanya ufuatiliaji wa karibu kwa wanufaika wa mikopo ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Huku akiwataka wanufaika kurejesha mikopo kwa wakati, hivyo kutoa fursa kwa wengine kunufaika na mfuko huo na kuendeleza mzunguko wa uwezeshaji kiuchumi.
Kwa upande wa benki zilizotambuliwa, wawakilishi wake wamesema kuwa wamepewa jukumu hilo na watalitekeleza kwa weledi na kasi, kwa kushirikiana na maafisa mikopo wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Serikali iliisimamisha mikopo hiyo ya 10% ili kufanya maboresho, na sasa imechagua Halmashauri 10 za mfano, ikiwemo Jiji la Dar es Salaam na tayari imeingia makubaliano na benki mbili ya CRDB na benki ya NMB kwa ajili ya utoaji wa mikopo hiyo, huku shilingi bilioni 15 zikiwa zimetengwa kwa ajili ya Mikopo kutoka kwenye mapato ya ndani na marejesho ya mikopo ya awali. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa wanufaika wanapata fursa bora zaidi za mikopo kwa maendeleo yao.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.