Na: Hashim Jumbe
TAREHE 5 Juni, 2021 Watanzania tutaungana na Nchi mbalimbali Duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliamuliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa la mwaka 1972, wakati wa mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu Mazingira huko Stockholm, nchini Sweden.
Kuelekea Siku ya Mazingira Duniani, ambayo itakuwa ni tarehe 05 Juni, 2021 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo wamefanya usafi katika Zahanati ya Vingunguti ikiwa ni Siku ya kwanza ya ufunguzi wa wiki ya mazingira iliyoanza leo tarehe 01 Juni, 2021 na itaendelea mpaka siku ya kilele ambayo ndiyo itakuwa Siku ya Mazingira Duniani.
Itakumbukwa kuwa, dhumuni kuu la maadhimisho haya ya Siku ya Mazingira Duniani ni kuhamasisha Jamii zetu kuelewa masuala yanayohusu Mazingira na pia kuwahamasisha Watu kuwa mstari wa mbele katika kuchukua hatua za uhifadhi na kulinda mazingira "Wilaya ya Ilala inatoa wito kwa kila Mwananchi kushiriki kwenye shughuli za usafi na uhifadhi wa Mazingira kwa kupanda miti na kusafisha Mazingira ya maeneo yao ya majumbani na mitaa wanayoishi" Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija, akitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari
Kwa mwaka huu wa 2021, kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira ni 'Tutumie nishati mbadala kuongoa mfumo ikolojia' Kaulimbiu hii inahimiza juu ya mustakabali wa Afya na Usalama wetu utategemeana na kiwango cha uwekezaji tunachofanya kwenye usimamizi na uhifadhi wa mazingira yetu.
Aidha, kwa wiki hii ya Mazingira Duniani, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepanga kufanya usafi na uhamasishaji wa utunzaji wa Mazingira katika Zahanati ya Vingunguti, Kutoa elimu ya utunzaji wa Mazingira kwa Shule za Msingi Kumi (10) kufanya usafi na kuhamasisha utunzaji wa Mazingira katika Mfereji wa Buguruni Malapa, kupanda miti na kuhamasisha upandaji wa miti, bonanza la michezo na mwisho itakuwa ni kilele cha Maadhimisho yatakayoambatana na maonesho ya wadau mbalimbali wa utunzaji wa Mazingira, kilele kitakuwa Viwanja vya Mnazi Mmoja.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.