Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Jiji la Hamburg leo Novemba 27, 2023 wamezindua warsha ya siku 5 kwaajili ya kuendeleza dhana ya ukarabati wa bustani ya mimea (Botanical Gurden) Jijini Dar es Salaam iliyoambatana na kauli mbiu isemayo ‘Together Pamoja Gemeinsam’.
Akizindua warsha hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kivukoni Bw. Majula Mtalemwa amesema “Tunawashukuru sana wenzetu wa Hamburg kwa kuja na mradi huu wa kuboresha bustani yetu ya Mimea kwani kutokana na uboreshaji huo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tutajifunza kutoka kwa wenzetu wa Hurmburg kuendesha bustani hii kwa faida na sio hasara hivyo tunaamini tunaweza kuanzisha huduma ndani ya Bustani ya Mimea ambazo zitaenda kutuongezea mapato kwa Halmashauri yetu, pia niwahamasishe wananchi wafike katika warsha hii ili waweze kujifunza zaidi jinsi ya kutunza mazingira.”
Kwa upande wake Kansela wa Seneti wa Jiji la Hamburg ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo na Ushirikiano wa Miji Dada Dkt. Anna Catarina Cebode ameeleza kuwa “Tumekubaliana kuimarisha eneo la bustani ya Mimea ya Dar es Salaam ambapo tutaboresha bustani hii na ndio maana leo hii tuko hapa kuhakikisha tunaweka mikakati mizuri ya kupendezesha bustani ya mimea ambayo kwa miaka michache mbele itakua bustani bora na yakujifunzia kwa watu wengine."
Naye Mkurugenzi wa Bustani ya Mimea Jijini Hamburg Prof. Dkt. Dominick Bergerow ameeleza kuwa timu ya wataalamu kutoka Hamburg itashirikina na timu ya wataalamu kutoka Jiji la Dar es Salaam ili kuhakikisha bustani ya mimea inaboreshwa ambapo sio bustani tu ila kutakua na usimamizi dhabiti wa maji katika bustani hiyo huku akisisitiza wananchi kushiriki kikamilifu siku ya Desemba Mosi ili kujifunza namna ya kutunza manzingira na nini kinaenda kufanyika katika Bustani ya mimea katika Jiji la Dar es Salaam.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.