NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Milao ameupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kulitoa jengo la kale la Old Boma ambalo lina zaidi ya miaka 160 liweze kutumika kama Kituo cha Urithi wa Ubunifu wa Majengo na Utalii.
Jengo la Old Boma lenye historia kubwa katika nchi yetu ambalo limefanyiwa ukarabati kwa kiwango cha juu na kuwa mfano wa uhifadhi endelevu na kituo cha kutangaza historia ya ukuaji wa miji yetu kanda ya Afrika Mashariki kwa ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya.
Akizungumza katika hafla ya kufungua kituo hicho leo Jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.Harrison Mwakyembe (MB), Milao alisema hatua hiyo inadhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa utamaduni wa Mtanzania unadumishwa na kukuzwa.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Waheshimiwa Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji Isaya Mwita Charles, Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya, Balozi wa Ufaransa, wananchi na wadau mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam.
Mgeni rasmi pia amesifu juhudi zinazofanywa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam za kuvitangaza vivutio vya utalii jijini kwa lengo la kuogeza pato kupitia shughuli za utalii na mipango yake ya kuwa na mabasi ya Halmashauri ya kuhudumia watalii.
Bi. Nuru pia ametoa pongezi kubwa kwa Jumuiya ya Wabunifu Majengo Tanzania na washirika wake kwa juhudi wanazofanya za kuanzisha mpango wa kuelimisha, kutunza na kudumisha majengo ya kale ambayo utakua ukisaidia kukuza na kuendeleza utalii katika Jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.
Akihitimisha hotuba yake mgeni rasmi ametoa wito kwa wananchi na wadau wote kuwa na mawazo ya utunzaji wa majengo ya kale badala ya uvunjwaji wa majengo hayo kama inavyoendelea katika Jiji la Dar es Salaam bila kupata vibali vya mamlaka husika Serikalini.
Mgeni rasmi ametoa msisitizo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Jiji la Dar es Salaam wa kusimamia sheria na kushughulikia kero zinazotokana na udhaifu wa kutosimamia sheria ambazo kimsingi zingeweza kusaidia kuimarisha usalama na kutunza mazingira ya majengo yote ya kale na majengo ya kisasa ambayo ni sehemu kubwa ya vivutio vya utalii nchini.
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Isaya Mwita Charles ameeleza kuwa kufunguliwa kwa kituo hiko ni fursa ya kukuza pato la uchumi la wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na taifa kwa ujumla kupitia mapato ya watalii watakaokitembelea.
"Tayari tumeweka mipango mbalimbali ya kukuza, kuhifadhi, kutangaza vivutio vya utalii tulivyonavyo na kuvifanya kuwa vyanzo vikubwa vya mapato katika Jiji letu ikiwemo utoaji mafunzo kwa madereva Teksi ambao wanahusika katika kuwasafirisha watalii ili wawe na uelewa zaidi kuhusu kituo hiki” alisema Mstahiki Meya wa Jiji.
Kwa Upande wake Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya Mhe. Roeland Van De Geer amesema ofisi yake iko tayari kushirikiana kwa karibu na Jiji la Dar es Salaam na Tanzania katika kukuza na kuendeleza majengo ya kale na katika kuleta maendeleo kwa ujumla.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.