Wajumbe wa Kamati za Nidhamu za Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC) kwa ngazi ya Wilaya wamehimizwa kuendelea kutekeleza jukumu la Msingi la kuhakikisha wanasimami Utumishi na Maadili ya Walimu ili kuwa na Walimu wenye kujituma na wanaozingatia maadili ya kazi yao kwaajili ya kuwalea watoto kwa usahihi na kuboresha elimu nchini.
Wito huo umetolewa leo Septemba 25, 2024 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Zainab Katimba (Mb) wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya wajumbe wa Kamati za nidhamu za Tume ngazi ya Wilaya yanayofanyika katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam kwa Kanda ya Mashariki iliyojumuisha Wilaya za Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Pwani na Morogoro.
Akiongea wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Katimba ameipongeza Tume ya Utumishi wa Walimu pamoja na wajumbe wake kwa utendaji mzuri wa kazi unaoambatana na uzoefu na uaminifu katika kutekeleza Majukumu yao.
"Nipende kutoa pongezi zangu kwa Tume pamoja na wajumbe wa Kamati kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuhakikisha mnateleleza majukumu ya kisheria pamoja na kusimamia utumishi wa Walimu kwani mafunzo haya yana lengo la kuwawezesha wajumbe wa Kamati kufahamu wajibu wao katika kusimamia ajira, nidhamu na maadili ya Walimu hivyo ni imani yangu mafunzo haya yatakua chachu ya kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya Tume na Serikali kwa Ujumla lengo likiwa ni kuendana na kauli mbiu ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhun Hassan ya 'Kazi Iendelee' na Sisi kama viongozi tutaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kazi ziendelee kufanyika kwa ufanisi na uadilifu." Amesisitiza Mhe. Katimba.
Awali akitoa salamu wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu Prof. Masoud Mureke ameeleza kuwa lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo wenyeviti na wajumbe wa Kamati za Tume za Wilaya ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi huku akiahidi kuwa Tume itaendelea kusimamia jukumu lake la msingi la usimamizi wa Utumishi na Maadili ya Walimu kwa lengo la kuhakikisha Walimu hao wanazingatia maadili kwa manuafaa ya watoto na kuendelea kuboresha Elimu Nchini.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Msaidizi wa Tume Wilaya ya Ilala Mwl. Subira Mwakibete ameeleza kuwa baada ya mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengee uwezo wajumbe wa Kamati za Tume za Wilaya ni imani kwao wataendelea kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuhakikisha sekta ya elimu nchini inakua na Walimu wanatimiziwa stahiki zao muhimu kwa wakati.
Aidha, Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku Siku mbili (2) kwa wajumbe wa wilaya 139 kwa Kanda tano (5) ambazo ni Kanda ya Kaskazini ambapo mafunzo yanafanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Jiji la Arusha kwa Wajumbe wa Wilaya za Mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga, Kanda ya Mashariki ambapo mafunzo yanafanyika katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam kwa Wajumbe wa Wilaya za Mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, Kanda ya Kati ambapo mafunzo yanafanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora katika Manispaa ya Tabora kwa Wajumbe wa Wilaya za Mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora, Singida, Tabora na Dodoma, Kanda ya Ziwa ambapo mafunzo yanafanyika katika Ukumbi wa Nyakahoga Jijini Mwanza kwa Wajumbe wa Wilaya za Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Geita pamoja na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambapo mafunzo yanafanyika katika Ukimbi wa Dkt. Shein Jijini Mbeya kwa Wajumbe wa Wilaya za Mikoa ya Rukwa, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa na Mbeya.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.