Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewasihi wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuendelea kupanda miti na kutunza mazingira kama ishara ya kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Mpogolo ameyasema hayo leo 25 Novemba, 2023 mara baada ya kupanda miti akishirikiana na Viongozi pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mnyamani, zoezi ambalo limekwenda sambamba na zoezi maalumu la usafi wa Kila mwisho wa mwezi lililofanyika katika Kanda namba tatu, Kata ya Mnyamani Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
“Miti ni ishara ya uhai, Watoto na Viongozi hawa waliopanda miti wameungana na Mhe. Rais kuleta uhai wa watu wa Kata hii, hivyo tuendelee kupanda miti kama ishara ya kumuunga mkono Rais wetu katika suala la utunzaji wa mazingira.”
Sambamba na hayo, Mhe. Mpogolo amewapongeza viongozi wote wa Kanda namba tatu kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya katika usafi na utunzaji wa mazingira na kutoa wito wa kusimamia na kuendeleza usafi wa mara kwa mara katika maeneo yao kwani kuna baadhi ya maeneo watu wameyageuza kuwa majalala hivyo kuhatarisha afya za wakazi wa maeneo husika.
Naye Diwani wa Kata ya Mnyamani Mhe. Shukuru Dege amewapongeza wote walioshiriki katika zoezi hilo la usafi na kusema kuwa wao kama kanda namba tatu wamejipanga kutosubiri kufanya zoezi hilo mwisho wa mwezi bali watalifanya kila jumamosi kwa kuchagua mtaa mmoja na kufanya usafi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.