Na: Rosetha Gange
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Ndg. Hassan Rugwa ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es salaam kupima afya zao mara kwa mara ili waweze kuzijua afya zao na hatimaye waweze kutokomeza UKIMWI na magonjwa ya mlipuko.Ndg. Rugwa ameyasema hayo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo kwa Mkoa wa Dar es salaam yamefanyika katika viwanja vya shule ya msingi Miembeni iliyopo Kata ya Vingunguti, Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam.
Kwa mwaka huu wa 2021 maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo ‘Zingatia usawa, tokomeza UKIMWI, tokomeza magonjwa ya mlipuko’ ambapo inasisitiza ushiriki na ushirikishwaji wa jamii katika shughuli za kudhibiti UKIMWI kuanzia kwenye upangaji wa mikakati, upatikanaji na utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI ndani ya Mkoa wa Dar es salaam, hivyo wote kwa pamoja tunao wajibu wa kushirikiana kuhakikisha tunatokomeza UKIMWI na magonjwa yote ya mlipuko kwa kuzingatia maagizo yote tunayopewa na wataalamu wa afya.
Aidha Ndg. Rugwa anasema “Tuzingatie elimu tunayopewa, tuendelee kubadili tabia na mila zinazochochea maambukizi ya VVU ili tuendelee kulinusuru Taifa letu na familia zetu na kuepuka unyanyapaa, unyanyasaji na ubaguzi kwani hivi vinakwamisha jitihada za Serikali na wadau katika kupambana na VVU".
Pamoja na hayo Ndg. Rugwa amesema kuwa katika Mkoa wa Dar es salaam shughuli mbalimbali zimekuwa zikifanywa katika kupambana na VVU na UKIMWI ikiwemo kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi mapya ya VVU kwa jamii na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, kupunguza unyanyapaa na vitendo vya unyanyasaji na ubaguzi unaohusiana na maambukizi ya VVU, kutoa ushauri nasaha pamoja na kupima VVU kwa hiari, kuzuia maambukizi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto, kutoa tiba ya magonjwa nyemelezi, kutoa dawa za kufubaza VVU n.k.
Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani hufanyika kila ifikapo tarehe 1 Desemba na kwa mwaka huu yameadhimishwa Kitaifa katika Jiji la Mbeya ambapo kauli mbiu iliyosindikiza maadhimisho haya nchini kote ni Zingatia Usawa, Tokomeza UKIMWI, Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.