Wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam wametakiwa kuwa mabalozi katika matumizi ya Nishati Safi na salama ya kupikia,lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za utunzaji wa Mazingira.
Wito huo umetolewa na Mshauri wa Rais katika masuala ya wanawake na makundi maalumu Dkt. Sophia Mjema, wakati wa Mkutano wa Uzinduzi wa Programu ya ‘Imarisha Uchumi na Mama Samia’ (IMASA) iliyofanyika Leo Mei 22, 2024 katika Ukumbi wa Arnatoglou Jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha viongozi mbalimbali wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoa wa Dar es Salaam, Taasisi na Mashirika binafsi.
Aidha, Dkt. Mjema amesema "Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila Mkoa, Wilaya, Kata na Mitaa kunakuwa na sehemu ambapo wananchi wataweza kupata nishati Safi na salama ya kupikia kwani kupitia nishati safi tutahakikisha usalama, uendelevu na urahisi wa upatikanaji wa nishati ya kupikia, kuokoa muda, pamoja na kupunguza gharama za matumizi, athari za kimazingira na kiafya kwa watumiaji. Pia, ni nyenzo muhimu katika kutekeleza makubaliano ya kitaifa na kimataifa yanayolenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza uzalishaji wa gesi joto”.
Sambamba na hilo, Dkt. Mjema amemshukuru Rais Jamhuri ri ya Muungano wa Tanzania kwa kuja na mkakati wa matumizi safi ya nishati ya kupikia huku akiwashukuru Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kuja na Programu ya ‘Imarisha Uchumi na Mama Samia’ ambayo itakua chachu ya kuwakutanisha wanawake na wananchi katika kujadili masuala mbalimbali ya Kiuchumi bila kusahau suala la nishati safi ya kupikia.
Awali akiongea wakati wa Mkutano huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Toba Nguvila amesema “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Jamhuri ri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa na maono ya kuwakwamua wananchi kiuchumi kwani Mkoa wa Dar es Salaam uko tayari katika kutekeleza programu hii ya IMASA inayolenga kutambua na kuwezesha shughuli za Kiuchumi na ukizingatia Dar es Salaam ni Mkoa wenye fursa za kiuchumi na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi hivyo kuja kwa programu hii katika Mkoa wetu ni fursa kwetu hivyo ninawahakikishia ushirikiano katika kutekeleza mpango huu na nitoe wito kwa wanawake na makundi maalumu kushiriki kikamilifu katika hili kwani huu ni wakati muafaka kwenu wa kujikwamua kiuchumi”.
Naye, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Bengi Issa ameeleza kuwa mpango huo unafungua milango kwa wanawake kutambulika rasmi wao na biashara zao na mahali wanapofanyia shughuli zao za kibiashara kwani biashara nyingi ndogondogo za wanawake sio rasmi na wengi hawana leseni hivyo kupitia mpango huu wanawake watawaweza kujikwamua kiuchumi kwani watapatiwa mikopo kwaajili ya kukuza mitaji yao.
“Pamoja na mambo mengine mpango huo utaweza kutengeneza kanzidata ya kupata takwimu za wanawake hapa nchini na hizo ni juhudi za Serikali za kuanzisha programu hii ambayo itasimamiwa na baraza ili kuweza kuwapa elimu kuhusu mambo ya kodi, biashara , ujasiriamali , kanuni na sheria mbalimbali hapa nchini”. amesema Bi. Issa
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.