Maafisa Watendaji wa Kata, Mitaaa pamoja na Wenyeviti wa Mitaa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wametakiwa kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi kwa weledi kwa kuzingatia uadilifu na maadili ya Utumishi wa Umma.
Maagizo hayo yametolewa Leo Juni 27, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo wakati wa kikao kazi cha kukumbushana majukumu ya kazi zao, maadili ya utumishi wa umma sambamba na usimamizi wa miradi inayotekelezwa katika Halmashauri kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Shaaban Robert Uliopo Upanga Jijini Dar es Salaam.
Aidha Akiongea katika kikao hicho Mhe. Mpogolo amewataka Watendaji wa Kata, Mitaa pamoja na Wenyeviti wa Mitaa kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano pamoja na kujenga mahusiano mazuri na wananchi, Madiwani pamoja na viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi lengo likiwa ni kutekeleza Ilani ya Chama pamoja na kutambua kazi kubwa anayoifanya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora kwa ukaribu na uharaka zaidi.
Sambamba na hilo Mhe . Mpogolo amesema “Napenda kuwapongeza wote kwa kazi Nzuri mnazozifanya za kusimamia miradi pamoja na kuhudumia wananchi licha ya changamoto ndogondogo zinazowakabili Ila nipende kuwakumbusha mfanye kazi zenu kwa uadilifu msijihusishe na kazi za ukusanyaji wa mapato kwani sio kazi zenu hivyo mtekeleze majukumu yenu ya kuwahudumia Wananchi kwa ukaribu zaidi ili kutekeleza adhma ya Rais wetu ya kuhakikisha kila Mwananchi anapata huduma bora kwa wakati”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Ndg. Jomaary Mrisho Satura aliweza kuwapongeza Watendaji pamoja na Wenyeviti kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwahudumia wananchi katika maeneo yao huku akiwakumbusha kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu hasa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu na maelekezo maalumu ya Serikali.
“Kikao kazi hichi kina lengo la kuwakumbusha wajibu na majukumu yenu katika kusimamia mapato pamoja na utekelezaji wa miradi kwani imani yangu ni kuwa kila mtu anaomuongozo wa majukumu anayopaswa kutekeleza kila siku, kila mtu anafahamu sheria, kanuni na taratibu za kazi lakini zaidi zingatieni na kutekeleza maagizo yanayoshushwa kwenu, kwa kutoka ofisi ya Mkurugenzi, kwa kutambua kuwa mnaowajibu wa kufanyakazi kwa niaba ya Mkurugenzi katika maeneo yenu." Amesisitiza Ndg. Satura.
Akifunga Kikao hicho Mastahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto amesema “Tumedhamiria kubadilisha Jiji letu hivyo fedha zinapotolewa zitumike kwa uangalifu na kwa uaminifu ili kufikia malengo hivyo tuwe waadilifu katika kusimamia utekelezaji wa miradi yetu pia kwa kushirikiana Mkurugenzi tutahakikisha tunasimamia vyema majukumu yetu ikiwa ni kusimamia vyema utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji letu”.
Hata hivyo Maafisa Watendaji hao, wameushukuru uongozi wa Halmashauri kwa kikao kazi hicho chenye tija na kuahidi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi katika maeneo yao.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.