Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (Mb) leo tarehe 31 Mei, 2018 amezindua rasmi maonyesho ya Wiki ya Mazingira katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake ni tarehe 5 Juni, 2018.
Akizindua rasmi maonyesho hayo Waziri Mkuu alieleza sababu za kuchagua Jiji la Dar es Salaam katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kitaifa kwa mwaka 2018 kuwa ni pamoja na historia na changamoto nyingi za mazingira zinazolikabili Jiji hili ambalo ni kitivo na kitovu cha shughuli zote za uchumi nchini Tanzania.
Waziri Mkuu ametoa pongezi kwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa jitihada inazofanya za kuwawezesha wajasiriamali wadogo kuanzisha viwanda vya nishati mbadala ili kupunguza matumizi makubwa ya nishati ya mkaa ambayo yamesababisha kiasi kikubwa cha misitu yetu kuteketezwa na ametoa wito kwa Halmashauri za Miji, Wilaya, Manispaa na Majiji nchini kuiga jitihada za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika kuwawezesha wajasiriamali kuanzisha viwanda vya nishati mbadala.
Aidha Waziri Mkuu ametoa wito kwa Mikoa yote, Taasisi za Serikali na za binafsi kote nchini pamoja na wananchi wote kwa ujumla kuadhimisha siku hii kwa vitendo hususan kwa kufanya shughuli za uhifadhi wa mazingira katika maeneo ya makazi, maeneo ya mikusanyiko na mjumuiko ili mazingira yawe safi na salama.
Kwa upande wake kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo ameeleza kuwa kwa mujibu wa Takwimu za hadi kufikia mwaka 2017 zinaonesha kuwa kiasi cha hekta 46,942 za msitu kimekuwa kikiteketezwa kila mwaka na matumizi makubwa yakiwa ni nishati ya mkaa, na inakadiriwa kuwa Jiji la Dar es Salaam linatumia wastani wa tani 500,000 ya mkaa kila mwaka kiasi ambacho kinakadiriwa kuongezeka sana kutokana na ongezeko kubwa la watu kwa kila mwaka.
Mhandisi Ndikilo aliendelea kueleza kwamba Mkoa wa Dar es Salaam unakabiliwa na changamoto mbalimbali za uharibifu wa mazingira zikiwemo mafuriko, athari za mabadiliko ya Tabianchi zinazosababisha kuongezeka ujazo wa bahari na mawimbi makubwa yanayosababisha kubomoka kingo za bahari.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira yaliamuliwa mwaka 1972, katika mji wa Stockholm nchini Sweden, kwenye mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu Mazingira. Wakati wa mkutano huo Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia Mazingira Duniani, yaani United Nation Environment Programme, UNEP, lilipitishwa tarehe 5 Juni. Tangu wakati huo, nchi mbalimbali zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, tarehe 5 Juni ya kila mwaka, kwa ujumbe maalumu unaotolewa na Umoja wa Mataifa.
Kimataifa maadhimisho haya yana kaulimbiu isemayo “Beat Plastic Pollution”. Kaulimbiu hii inahimiza jamii kuepuka uchafuzi wa Mazingira utokanao na plastiki. Maamuzi ya kupeleka maadhimisho haya nchini India ni kutokana na nchi ya India kuweka juhudi katika kupunguza uchafuzi wa Mazingira utokanao na plastiki kwa kutumia mbadala wa plastiki na kurejeleza taka za plastiki. Aidha, India ni moja ya nchi zilizo mstari wa mbele katika kurejeleza taka za plastiki ukilinganisha na nchi nyingi duniani.
Kitaifa maadhimisho haya yanafanyika jijini Dar es Salaam, Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Mkaa Gharama; Tumia Nishati Mbadala”. Kaulimbiu hii inahimiza jamii kupunguza matumizi makubwa ya Nishati ya mkaa ambayo yamesababisha kiasi kikubwa cha misitu yetu kuteketezwa.
Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali pamoja na wananchi wameshiriki maonyesho hayo na kupata fursa ya kuona, kujifunza na kuwa na uelewa mkubwa wa namna ya kutumia nishati mbadala badala ya kuwa na matumizi makubwa ya nishati ya mkaa.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.