ZIARA YA MKUU WA WILAYA YA ILALA KATIKA KATA YA PUGU - GONGO LA MBOTO YATOA NJIA UTATUZI WA CHANGAMOTO YA MAJI.
Na Amanzi Kimonjo.
Mkuu wa wilaya ya Ilala Mhe.Ngw’ilabuzu Ndatwa Ludigija tarehe 26 mei 2021 ametembelea mradi wa ujenzi wa tanki na mfumo wa usambazaji wa maji uliopo Pugu-Gongolamboto Jijini Dar Es Salaam tenki ambalo linachukua ujazo wa lita milioni mbili ambalo limeshakamilika kwa asilimia mia moja na zoezi la usambazaji wa maji umeanza kwa kata ya Pugu maeneo ya Buyuni, Majoe, Gongo la mboto, Pugu Stesheni,na sehemu ndogo ya Chanika huku wananchi wakifurahia huduma ya maji na baadhi yao wako katika utaratibu wa kusambaziwa maji.
Hata hivyo, Mradi huu unaotoa bomba kuu la kusambaza maji lenye urefu wa kilomita 13.5 kutoka Kisarawe mpaka Ukonga Air wing pamoja na tenki lenye ujazo wa lita milioni mbili likiambatanishwa na mabomba madogo yenye upana wa ‘inch’ tatu hadi nane ya kusambaza maji katika Kata hizo yakiwa yamekamilika kwa asilimia mia moja.
Aidha, Mkuu wa wilaya Mhe. Ludigija amesema “Natoa pongezi kwa Mamlaka ya Maji Safi na Salama Dar es Salaam (DAWASA) kwa kuwezesha usimamizi na taratibu za usambazaji wa maji, kubwa zaidi kwa Wilaya ya Ilala ninatamani mradi huu uwe sehemu ya wananchi kupata maji na kuondokana na adha ya maji”. Hivyo tatizo la muda mrefu la ukosefu wa maji kwa kata ya Pugu-Gongolamboto litakua historia baada ya mda mchache.
Vile vile, Msimamizi wa mradi huu Mhandisi Ishumaili Kakwezi amesema “usambazaji wa maji unaendelea kwa mahitaji ya wateja na mpaka sasa tumewafikia wateja 2000 na wengine tunawaungia mabomba lengo huduma hii ya maji iwafikie kwa uharaka”.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Wilaya Mhe.Ludigija alitembelea mradi wa ujenzi wa daraja la Ulongoni A na Ulongoni B iliyoko chini ya mradi mkubwa wa DMDP ambapo ujenzi wa daraja la Ulongoni A uliogharimu shilingi billion 4.5 umefikia asilimia 79 na inategemewa kufikia mwezi wa sita wananchi wataanza kutumia daraja hilo, huku daraja la Ulongoni B lililo gharimu takribani shilingi billion 2.5 ujenzi bado unaendelea.
“Ninamshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, wataalamu wetu wakiongozwa na Mhandisi Magori, Mkandarasi na wengine walioshiriki katika kufanikisha ujenzi huu kwa hatua ulipofikia maana naona matumaini kua ifikapo tarehe 10 mwezi wa sita wananchi wataanza kutumia daraja hili na inafahamika mradi huu utamalizika tarehe 30 mwezi wa sita na nitoe wito kwa wataalamu wa Jjiji,mkurugenzi,mkandarasi,Tarura, waongeze kasi ya ujenzi huu nafarijika kuona jinsi kazi inavyoendelea na tutafuatilia mpaka hapo mradi huu utakapo malizika”.
Akitoa shukrani zake kwa viongozi Mhandisi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mhandisi .Magori amesema “Mradi huu wa ujenzi wa Daraja la ulongoni unaendelea na kwa niaba ya Halmashauri tunamshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa kuendeleza mradi huu pamoja na viongozi wetu Wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na Katibu tawala wa Wilaya ya Ilala kwa kuonyesha ushirikiano wao wa kutembelea na kuifatilia miradi hii toka imeanza mpaka hapa ilipofikia”.
Ziara hii ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala iliweza kumalizika kwa kutembelea ujenzi wa stendi ya Kinyerezi unaombatana na ujenzi wa barabara kutoka ulongoni B hadi kufika katika stendi hiyo ya Kinyerezi ambapo barabara hiyo yenye kilometa 9.5 ikiwa inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
Ukamilifu wa Stendi hii ya Kinyerezi ambayo ni kitovu cha biashara na shughuli nyingine za kiuchumi inategemewa na wananchi wa Kinyerezi pamoja na wananchi wa maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es salaam kwani ipo karibu na stendi kuu ya mabasi ya kwenda mkoani (Stendi ya Magufuli )hivyo basi itarahisisha wananchi wote wa Ilala kuweza kufika na kupata huduma.
Akihitimisha ziara yake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ludigija amesema “Mkandasi pamoja na wasaidizi wake wasibweteke kwa sifa hizi tunazowapatia bali wafanye kazi na waongeze kasi wasiseme Mkuu wa Wilaya amepita na kazi isimame nataka hadi kufikia tarehe 30, Juni 2021 kazi hii iwe imekamilika kama ilivyokusudiwa.”
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.