Na: Muandishi wetu
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo tarehe 07 Septemba, 2022 limefanya kikao chake cha kawaida cha kupitisha taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2021/2022 iliyoanza Aprili na kuisha Juni 2022.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mstahiki Meya, Mhe. Omary Kumbilamoto kimefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Arnatouglou kilianza na ajenda ya maswali ya papo kwa papo ambapo madiwani wametaka kutambua ni lini Halmashauri itaweka mkakati mzuri wa kuwaondoa wamachinga pembezoni mwa barabara kwani inaonekana wamachinga hao wamerudi katika maeneo waliyoondolewa.
Akijibu swali hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Tabu Shaibu amesema “tayari Halmashauri imefanya tathmini na wametafuta kampuni binafsi ambayo itasimamia zoezi hilo”.
Mbali na ajenda hiyo, hoja nyengine iliyojadiliwa ni kuhusu chanjo ya mifugo, ukarabati wa barabara ya kuingia machinjio na Halmashauri kuichukua timu ya mpira ya Dar City.
Aidha, ajenda nyingine ni uwasilishaji wa taarifa za utendaji kazi wa kamati za kudumu za Halmashauri ambazo ni kamati ya fedha na utawala, uchumi na huduma za jamii, mipango miji na mazingira na kamati ya kudhibiti UKIMWI, ambapo Baraza la Madiwani lilijadili na kupitisha taarifa hizo za robo ya nne ya mwaka wa fedha 2021/2022 iliyoanzia Aprili hadi Juni, 2022.
Naye, Meneja wa TARURA, Injinia Sylivester Chinengo akizungumza wakati wa kikao hicho cha Baraza la Madiwani alielezea juu ya ukarabati unaofanywa wa baadhi ya barabara zilizopo ndani ya Jiji la Dar es Salaam ambapo pia amemshukuru Mkurugenzi wa Jiji kwa ajili ya kiasi cha shilingi bilioni 6.22 zilizotengwawa kufanikisha ukarabati wa barabara hizo “Kwa niaba ya TARURA naomba kumshukuru Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kwa kutuunga mkono katika kukarabati barabara zetu, kiasi hiki ni kikubwa na kitatusaidia kutoka hatua moja kwenda nyingine.” Amesema Chinengo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.