Na: Hashim Jumbe, Judith Damas
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija, leo tarehe 10 Juni, 2022 amefungua Mashindano ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) ufunguzi uliofanyika kwenye Viwanja vya Ukonga Magereza.
Mashindano hayo yaliyoanzia kwa kushindanisha wanafunzi kuanzia timu za madarasa, shule, kata na kutengeneza timu za majimbo matatu, ambayo ni Jimbo la Ukonga, Jimbo la Segerea na Jimbo la Ilala, yanajumusha michezo kama vile mpira wa miguu, mpira wa wavu, mpira wa kikapu, mpira wa mikono, mpira wa pete, riadha na fani za ndani
Akizungumza katika ufunguzi wa mashindano hayo Afisa Michezo kutoka Idara ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dar es Saalam, Bibi Minja ameeleza kuwa kuelekea fainali za UMISSETA zitakazofanyika Agosti, 2022 Mkoani Tabora, timu ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imewaandaa vizuri wanafunzi kushiriki katika mashindano lengo likiwa ni kuhakikisha wanapeleka wanafunzi wengi ngazi ya Mkoa ili kuunda timu bora ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha Bibi Minja alieleza kuwa "tofauti na changamoto za kiufundi na kifedha zinazotukabili lakini pia tumeweza kupambana kuhakikisha wanafunzi wetu wanafanya vizuri kwani mwaka 2021 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tuliibuka washindi wa kwanza Kimkoa katika mashindano haya ya UMISSETA hivyo nipende kumshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuwapa ridhaa ya kushiriki katika mashindano ya UMISSETA pamoja na kuwekeza fedha kwa ajili ya kukamilisha mashindano haya.
Akifungua mashindano hayo ya UMISSETA ngazi ya Wilaya Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mheshimiwa Ngw'ilabuzu Ludigija amewaasa wanafunzi kutia nia na juhudi katika michezo hiyo kwani michezo ni afya na ajira kwani mashindano haya ni msingi wa vipaji vijavyo katika Taifa letu la Tanzania. "Lengo la michezo hii ni kupata vijana wenye vipaji ambapo kama Taifa tunataka tuendeleze vipaji hivi na baadae tuwe na timu imara na kama ikiwezekana tushiriki katika mashindano mbalimbali ya AFCON na World Cup kama ilivyofanyika kwa dada zetu Serengeti Girls ambao wameweza kufuzu mashindano ya World Cup hivyo sisi tuliochaguliwa tujiandae tuongeze bidii na juhudi ili tusijinyime fursa ya ajira kwani hapa ndio tunapoonesha vipaji vyetu." ameeleza Mheshimiwa Ludigija.
Sambamba na hilo Mheshimiwa Ludigija amewataka wanafunzi hao wacheze kiufundi na kiustarabu ili wasije wakaumizana kwani baada ya michezo hii wanatakiwa kurudi shule na kuendelea na masomo. "Lengo letu ni kuibua vipaji kwa vijana wetu hivyo nawaasa mkicheza mhakikishe mnacheza kiufundi na kiustarabu isije ikatokea kuumizana kwani baada ya mashindano haya mnatakiwa kuendelea na masomo kwani michezo ni mojawapo ya kuifanya akili yako kuwa imara kwahiyo baada ya hapa watakaochaguliwa inabidi mkaoneshe ujuzi wenu na wale itakaotokea mmebaki msikate tamaa mrudi shule na msome kwa bidii kwani michezo na elimu ni vitu vinavyoendana
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.