Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ngw'ilabuzu Ludigija ameridhishwa na kasi ya miradi inayotekelezwa na kusimamiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam huku akitoa Maelekezo kwa viongozi wanaosimamia miradi hiyo, hayo yamebainishwa katika muendelezo wa ziara yake aliyoifanya leo tarehe 05 Octoba,2022 ya kutembelea miradi ya maendeleo ikiwemo Ujenzi wa Vituo vya Afya na miundombinu mbalimbali inayotekelezwa na kusimamiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Aidha miradi iliyoweza kutembelewa Katika ziara hiyo ni pamoja na ujenzi wa Soko la Kigogo Fresh, Ujenzi wa Kituo cha Afya Kinyerezi, Ujenzi wa Kituo cha Afya Segerea pamoja na shule ya Sekondari Liwiti ambapo ujenzi wa soko la Kigogo Fresh lilogharimu takribani shillingi bilioni 2.6 ikiwa ni fedha za UVIKO- 19 linatarajiwa kukamilika ndani ya wiki tatu huku ujenzi wa kituo cha afya Kinyerezi kilichogharimu takribani kiasi cha shilingi milioni 500 ikiwa ni fedha kutoka mapato ya ndani na ujenzi uko asilimia 90 na hadi kufikia tarehe 30 Oktoba, 2022 ujenzi wa kituo hicho unategemea kukamilika pia ujenzi wa kituo cha afya Segerea pamoja na ujenzi wa shule ya Sekondari Liwiti ambayo inajegwa kwa fedha za mapato ya ndani pamoja na fedha za nje kutoka TAMISEMI takribani shilingi bilioni 1.4 hadi kukakamilika, jengo hilo lenye ghorofa tano linatarajia kukamilika hapo Desemba 2022 kwa ajili ya wanafunzi kuingia shule Januari 2023.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ludigija ameelekeza kua ni afadhali kuchelewa kukamilisha miradi hiyo ya vituo vya afya lakini tujenge vituo bora na vyenye viwango vinavyotakiwa hivyo amewaelekeza Viongozi wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam pamoja na wahandisi wanaosimamia miradi hiyo kuhakikisha inajengwa kwa viwango bora.
"Naelekeza kuwa wahandisi na wataalamu wetu wahakikishe wanadhibiti vifaa vinavyokuja kwenye maeneo ya ujenzi ni vilivyokusudiwa na vyenye ubora kwani tusipofanya hivyo miradi mingi itakua inakwama na haendi kama ilivyokusudiwa hivyo tuhakikishe magari yote yanayoleta mchanga na kokoto hayamwagi kwanza hadi tupime iwapo tani wanazozisema zinaendana na mzigo walioubeba hivyo namuagiza Mhandisi wa Halmashauri kuhakikisha anatembelea maeneo yote yanayojengwa kwakutumia Force Account ili kuhakikisha vifaa vyote vipo sawa na utekelezaji unatekelezwa kwa kiwango bora." Ameelekeza Mhe. Ludigija.
Sambamba na hilo Mheshiwa Ludigija amempongeza Pindoria Construction Co. Ltd kwa kazi nzuri anayoifanya ya ujenzi wa shule ya sekondari Liwiti pia amemtaka aendelee na juhudi hizohizo ili hadi kufikia DIsemba 2022 mradi huo uweze kukamilika ili wanafunzi waweze kuanza masomo ifikapo Januari 2023
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.