DC MPOGOLO AWAHAKIKISHIA WANANCHI ULINZI NA USALAMA KATIKA VITUO VYA KUJIANDIKISHA
Tarehe iliyowekwa: October 11th, 2024
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewasihi Wananchi wa Wilaya ya Ilala kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura la uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwani vituo vyote ni shwari ulinzi na usalama umeimarishwa na hakuna mtu yoyote wakuleta vurugu.
Mhe. Mpogolo ametoa wito huo leo Octoba 11, 2024 wakati akizindua zoezi la uandikishaji wa daftari la mpiga Kura la uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Mtaa wa Karume Kata ya Ilala Jijini Dar es Salam.
Akizungumza na Wananchi waliojitokeza kwenye zoezi hilo Mhe. Mpogolo ameeleza kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ilala imejipanga vyema kuhakikisha ulinzi unaimarika katika vituo vyote vya kujiandikishia.
"Nitumie nafasi hii kupongeza watu wote waliojitokeza katika kujiandikisha mimi na Viongozi wezangu tumefanya ziara na tunaendelea kufanya ziara katika vituo vyote vya kujiandikishia ambapo tumeona mutikio ni mkubwa sana na muitikio huu unaonesha jinsi gani mmewaelewa viongozi wenu pamoja na juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati na mpo tayari kuwapigia kura ifikapo Novemba 27, 2024 hivyo niwahakikishie ulinzi na usalama katika vituo vyote vya kujiandikisha na katika kipindi chote cha zoezi la kujiandikisha". Amesisitiza Mhe. Mpogolo.
Sambamba na hilo Mhe. Mpogolo ameeleza kuwa vituo vya kujiandikishia ni vituo zaidi ya 454 katika mitaa 159 ya Jiji la Dar es Salaam ambapo vituo vyote hali ni shwari na salama huku akiwataka wananchi hao kuwahamasisha wengine kujitokeza kujiandikisha pamoja na kuwasihi watu ambao wana viashiria vya uvunjifu wa amani kuacha mara moja kwani watachukuliwa sheria badala yake kila mmoja atekeleze wajibu wake katika kufanikisha zoezi hilo la uandikishaji.