Na Doina Mwambagi
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amewatoa wasiwasi wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuwahakikishia kuwa miradi ya maendeleo inayokaribia kukamilika itatekelezwa kwa wakati kama ilivyopangwa.
Ametoa kauli hiyo leo Juni 20, 2025 wakati wa uvunjaji rasmi wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lililokuwa likihusisha madiwani 36 pamoja na madiwani wa viti maalum 13.
Katika hotuba yake, DC Mpogolo amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam chini ya Mkurugenzi Mabelya ina watendaji makini, wenye maono na wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi na uwajibikaji mkubwa katika kusimamia maendeleo ya wananchi.
"Tuna imani kubwa na uongozi wa Mkurugenzi Mabelya pamoja na timu yake ya wataalamu. Wanajituma, wanafanya kazi kwa uaminifu na wamejipanga kuhakikisha miradi yote inaisha kwa ubora unaostahili," amesisitiza DC Mpogolo.
Sambamba na hilo, Mheshimiwa Mpogolo amempongeza Mstahiki Meya wa Jiji hilo, Omary Kumbilamoto, pamoja na Baraza la Madiwani kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri, kwani wao ndio sababu ya mafanikio yanayoonekana leo, na wananchi wanafurahia miradi hiyo inayogusa maisha yao moja kwa moja.
Hatua ya kuvunjwa kwa Baraza hilo la Madiwani inatekeleza agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa, aliyeagiza Halmashauri zote nchini kuvunja mabaraza ya madiwani ifikapo Juni 20, 2025, kufuatia kumalizika kwa muda wa kisheria wa uongozi wa Serikali za Mitaa.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.