Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewasihi wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuendelea kupanda miti na kutunza mazingira kama ishara ya kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Mpogolo ameyasema hayo leo 27 Januari 2024 mara baada ya kupanda miti ya matunda na vivuli akishirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Viongozi mbalimbali, Wananchi pamoja na wadau wa Mazingira kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zoezi ambalo limekwenda sambamba na zoezi maalumu la usafi wa Kila jumamosi ya mwisho ya mwezi.
“Miti ni ishara ya uhai, watu waliopanda waliopanda miti hii leo wameungana na Mhe. Rais kuleta uhai wa watu wa Wilaya yetu hii, hivyo tuendelee kupanda miti kama ishara ya kumuunga mkono Rais wetu katika suala la utunzaji wa mazingira. Hivyo tuhakikishe miti hii inatunzwa na inaleta manufaa kama ilivyokusudiwa." Amesema Mhe. Mpogolo
Halkadhalika, Mhe. Mpogolo amewataka wananchi kufanya usafi kama desturi yao na sio kusubiri mpaka mwisho wa mwezi ufike ili kuweka mazingira safi na kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linapendeza na kuwa safi, "Tuhakikishe kwamba usafi ni jambo la kwanza katika Wilaya yetu na ukilinganisha kwamba sisi ni Jiji Lazima tuendane na hadhi ya Jiji. Hivyo nipende kutoa shukrani zangu za dhati kwa kampuni zote zinazofanya kazi ya ukusanyaji na uzoaji wa taka kwani wanafanya kazi nzuri ya kuliweka Jiji letu katika hali ya usafi." Ameongeza Mhe. Mpogolo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amewapongeza na kuwashukuru wadau pamoja na taasisi mbalimbali ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha malengo ya Upandaji miti na usafi yanafanikiwa katika Halmashauri yetu na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Maeneo mengine yaliyopandwa miti ni pamoja na Shule za msingi Majani ya Chai, Buguruni Viziwi, Hekima, Moto Mpya, Kisiwani, St. Augustine, Furaha, Pugu Stesheni pamoja na Shule ya Sekondari Kiwalani na takribani miti elfu moja (1000) imepandwa katika maeneo hayo pamoja na usafi kufanyika kwenye kanda zote saba za kutolea huduma.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.