Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita leo tarehe 05 Oktoba, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na ugeni kutoka Taasisi ya mtandao wa Majiji zaidi ya 90 duniani inayoshughulika na namna bora ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabia ya Nchi Duniani “C40 CITIES” ofisini kwake Karimjee jijini hapa.
Ugeni huo uliwakilishwa na Mkurugenzi wa C40 CITIES Kanda ya Afrika, Hastings Chikoko na Mkurugenzi C40 CITIES Kanda zote duniani kutoka jijini London, nchini Uingereza.
Akizungumza mara baada ya kufanya mazungumzo na ugeni huo, Meya Mwita amesema kuwa wamejadili mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuboresha miundombinu yenye changamoto ya mafuriko, joto na usafiri jijini ili wananchi waweze kuepukana na athari za mabadiliko ya Tabia Nchi.
Amefafanua kuwa katika mazungumzo hayo Taasisi ya C40 imesema italeta mtalamu wa masuala ya Mabadiliko ya Tabia ya Nchi ambaye atafanya kazi kwa kushirikiana na wataalam wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam ili kupata namna bora ya kushughulikia athari hizo jijini Dar es Salaam.
Amesema mbali na hilo lakini pia wameahidi kutoa fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi ikiwemo kuboresha maeneo ambayo yanakumbwa na mafuriko kama Bonde la Mto Msimbazi, Jangwani na maeneo mengine.
Meya Mwita aliendelea kueleza kwamba Jiji la Dar es Salaam limekuwa likikabiliwa na changamoto kubwa ya mafuriko kipindi cha mvua jambo ambalo husababisha baadhi ya wananchi kupoteza maisha, huku wengine wakikumbwa na uharibifu mkubwa wa mali zao.
“Mji wetu unakuwa kwa kasi kubwa, tunatakiwa kujipanga mapema, maeneo mengi yanakumbwa na mafuriko wakati wa mvua, wananchi wetu wanahangaika, sasa imefika kipindi ambacho tunapaswa kulipatia ufumbuzi jambo hili” amesema Meya Mwita.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa C40 CITIES Kanda ya Afrika, Hastings Chikoko ameeleza kuwa Jiji la Dar es Salaam lilijiunga na Taasisi ya C40 tokea mwaka 2014 na wamekua wakishirikiana pamoja na kubadilishana ujuzi na uzoefu namna bora ya kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi hususani katika maeneo yanakumbwa na mafuriko, udhibiti wa taka ngumu na uboreshaji wa usafiri jijini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa C40 CITIES, Simon Hansen alieleza kwamba lengo la mazungumzo yake na Mstahiki Meya wa Jiji ni kuwa na ushirikiano wa pamoja kati ya Jiji la Dar es Salaam na Taasisi ya C40 ili kuandaa Mpango Kazi wa namna bora ya kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi ikiwemo mafuriko, joto, ukame na Jiji la Dar es Salaam kama Majiji mengine duniani kuwa na mchango katika kupunguza ongezeko la joto duniani kutozidi 1.5 nyuzi joto kiwango ambacho kikifikiwa Athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi Duniani zitapungua.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.