Jiji la Dar es Salaam limefanikiwa kuwa Jiji la sita kwa kuimarisha usafi wa mazingira ikilingwanishwa na miji mingine ya Afrika. Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija, amewaeleza wananchi kuhusu mafanikio hayo katika uzinduzi wa kampeni ya wiki ya mazingira duniani iliyoanza tarehe 02 Juni, 2022. Uzinduzi wa kampeni hiyo, ambayo kilele chake ni tarehe 05 Juni, 2022, umefanyika katika Kata ya Gerezani jijini Dar es Salaam.
“Kwa hatua hiyo ya mafanikio, wadau wa mazingira mmelipatia heshima Jiji la Dar es Salaam kwa kulifanya kuwa mojawapo kati ya majiji masafi barani Afrika kwa sababu kwa kutunza mazingira tunakuwa na afya bora na akili timamu inayotusaidia kutekeleza majukumu yetu vizuri, ” alisema Mhe. Ng’wilabuzu.
Mkuu huyo wa Wilaya aliwaelekeza wananchi kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya wiki ya mazingira isemayo “Tanzania moja tu. Tunza mazingira”, akisisitiza utunzaji wa mazingira uambatane na kazi ya upandaji wa miti ili kutimiza lengo la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam la kupanda miti milioni mbili na laki tano.
Mhe.Ludigija ameitumia fursa hiyo pia kuwapongeza wakandarasi wa usafi kwa kazi nzuri wanazozifanya kuimarisha usafi kupitia kampeni hiyo na kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi. Amewataka wakandarasi hao kuendelea na kazi zao bila kuchoka kwa kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ni taswira ya Tanzania kwa usafi.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omari Kumbilamoto, amempongeza Mkuu wa Idara ya Mazingira katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Rajabu Ngoda kwa kazi nzuri ya kuliweka Jiji safi kupitia Idara ya Mazingira.
Aidha, Mstahiki Meya amemuomba Mkuu wa Wilaya kuzifikisha salamu za wananchi wa Dar es Salaam kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwamba kwa takribani miaka sasa Jiji la Dar es Salaam halijawa na changamoto za magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
Katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri, naye aliwaambia wananchi kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imejipanga kufanya operesheni ya usafi kwa kuzingatia kwamba Jiji hilo ni kitovu cha shughuli nyingi. “Usafi unaanza na mimi. Timiza wajibu wako”, alisema Shauri akiahidi kuendeleza juhudi za kuimarisha usafi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.