Katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoambatana na athari za Kimazingira Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Maziringira kwa kushirikiana na Umoja wa Majiji Duniani (C40 Cities) pamoja na wadau wa Mazingira kutoka Taasisi zisizo za Kiserikali wamefanya Warsha ya siku mbili yenye lengo la kukabiliana na kuthibiti taka oza( Organic Waste) kwa Jiji la Dar es Salaam.
Warsha hiyo iliyoanza Septemba 25, na kuhitimishwa Septemba 26, imefanyika katika Hotel ya Holiday Inn Jijini Dar es Salaam ikiwahusisha wataalamu wa mazingira kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam, wadau wa mazingira kutoka UK, AID na British High Commission pamoja na Taasisi zisizo za Kiserikali.
Akiongea wakati wa warsha hiyo Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Theresia Denis ameeleza kuwa kutokana na changamoto ya taka oza (Organic Waste) kushika hatamu hususani maeneo ya masoko, Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na C40 Cities pamoja na wadau wa mazingira wameweza kuanzisha mradi jumuishi wa mabadiliko ya tabia ya nchi uliotekelezwa katika Mtaa wa Butiama Kata ya Vingunguti, Bonyokwa pamoja na Shule ya Sekondari Zanaki ambapo taka hubadilishwa kuwa chakula cha kuku na mbolea pamoja na kusaidia kupunguza athari za kimazingira zinazotokana hizo.
Kwa upande wake Mshauri wa Jiji-mabadiliko ya tabia nchi Bw. Jophillene Bejumula ameeleza kuwa lengo la warsha hii ni kuendelea kuweka mipango madhubuti na ya muda mrefu ya kuhakikisha hadi kufikia 2050 Jiji la Dar es Salaam lisizalishe hewa ya ukaa (Carbon) inayotokana na uzalishaji wa taka oza huku akitoa wito kwa wadau wengine wa mazingira kuendelea kutoa ushirikiano katika kutunza maingira kwa kuendelea kutenganisha taka ili kuepukana na magonjwa ya Mlipuko.
Naye Afisa Masoko Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bw. Alex Bubelwa amesema kuwa kutokana na warsha hiyo ni imani yake mradi wa kutenganisha taka oza utakua na manufaa makubwa katika kupunguza taka masokoni kwani taka za aina hizo huzlishwa masokoni na kipindi cha mvua taka hizo ni changamoto katika utunzaji wa mazingira hivyo mradi huo utakua chachu ya kuweka mazingira katika hali ya usafi.
Aidha, Akieleza umuhimu wa Mradi wa jumuishi wa mabadiliko ya tabia ya nchi uliotekelezwa katika Mtaa wa Butiama Kata ya Vingunguti Jijini Dar es Salaam, Afisa Afya Mkuu wa Kata hiyo Bw. Geophrey Zenda ameeleza kuwa mradi huo umekua chachu ya uboreshaji wa mazingira pamoja na kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa sambamba na kupungua kwa magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu.
Akitoa Shukrani zake kwa wadau wa mazingira Mnufaika wa mradi jumuishi wa mabadiliko ya Tabia ya nchi Bw. Michael Humbi ambae ni mwenyekiti wa Kikundi cha wazalendo Butiama ameeleza kuwa mradi huo umeweza kuwapatia ajira kwani kupitia mradi huo wameweza kuzalisha mbolea ya Mboji na wadudu kwaajili yanchakula cha kuku ambavyo ni chachu ya wao kupata kipato pamoja na kuendelea kutunza mazingira.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.