Wadau kutoka kada mbalimbali leo tarehe 22 Oktoba, 2020 wamekutana jijini Dar es Salaam kujadiliana matumizi ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Mbezi Luis ambacho ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 85.
Akisoma hotuba ya ufunguzi mbele ya wadau hao Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Sipora Liana amesema lengo la kikao hicho na wadau ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusiana na uboreshaji wa huduma ya usafiri na usafirishaji jijini Dar es Salaam hasa kwa mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani.
Mkurugenzi Sipora aliendendelea kufafanua kwamba, kupitia kikao hicho watapata fursa ya kusikia maoni, ushauri na mapendekezo kutoka kwa wafanyabiashara, wadau mbalimbali wa usafiri na usafirishaji na kwa pamoja wataweza kufikia lengo la utoaji wa huduma zenye ubora kwa mpangilio na utaratibu shirikishi ili kutengeneza mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na watoa huduma kufanya shughuli zao katika kituo hicho cha mabasi.
“Kituo kipya cha mabasi cha Mbezi Luis kitawezesha utoaji wa huduma bora ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi na wageni pamoja na kutoa fursa za biashara kwa wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo, baba na mama lishe ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato ya Serikali”, Alieleza Mkurugenzi wa Jiji.
Wadau mbalimbali waliohudhuria majadiliano hayo kwa pamoja wamepongeza jitihada za uboreshaji wa miundombinu ya utoaji huduma mbalimbali zinazotekelezwa pote nchini na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.