Kamati ya Ngozi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, yajipanga kuboresha zao la ngozi kuwa la Kibiashara zaidi, hayo yamebainishwa leo tarehe 31 Oktoba, 2023 na Wajumbe wa Kamati ya Ngozi wakati wa Ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kipindi cha Robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 ulioanza Julai hadi Septemba 2023.
Wakiwa kwenye ziara hiyo Wajumbe waliweza kutembelea eneo la uchakataji wa awali wa ngozi lililopo Ukonga Mazizini ambapo wajumbe waliweza kuangalia uchakati wa awali wa ngozi pamoja na kujifunza namna zao la ngozi linavyoandaliwa hadi kufikishwa sokoni.
Akiongea wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Ngozi Mhe. Moza Mwano ameeleza kuwa “Ngozi ni zao la ziada linalotokana na mifugo ambalo hutumika kama malighafi muhimu katika viwanda vya ngozi na huingiza fedha nyingi za kigeni kwani kutokana na maelezo ya mchakataji inakadiriwa kuwa asilimia 95 ya ngozi zote huuzwa nje hususani Nchini Nigeria na hutumika kama chakula hivyo kwa mazingira haya inabidi Kuboresha uzalishaji, ukusanyaji na usindikaji wa ngozi kwa ajili ya soko la ndani na nje ili kuongeza kipato kutokana na zao la ngozi."
Awali akitoa maelekezo ya namna ya uchakataji wa ngozi, Mchakataji wa ngozi Bw. Mogendi Kesele ameeleza kuwa kwa upande wake huchakata ngozi na kuuza nchini Nigeria kama chakula ambapo ngozi yenye kilo 14 huuzwa kwa shilingi elfu 10 mpaka elfu 15 huku ngozi yenye chini ya kilo hizo ikiuzwa elfu 7 mpaka elfu 10.
Aidha, kutokana na umuhimu wa zao la ngozi kibiashara, Kamati imependekeza Halmashauri itenge eneo nzuri la uchakataji wa ngozi pamoja na shughuli nyingine zinazozlishwa na kutokana na zao la ngozi kwani zao hilo litakua chachu ya ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.